Wednesday, November 5, 2014

HALMASHAURI MBINGA YATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA MAGARI YA ABIRIA

Mkurugenzi mtendaji, Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa onyo kali kwa wamiliki wa magari ya abiria kuhakikisha kuwa vijana wanaowatumia kupiga debe katika eneo la stendi kuu mjini hapa, kuacha kunyanyasa abiria kwani vitendo hivyo vinawadhalilisha na kuwanyima uhuru wa kuchagua basi walipendalo wakati wanaposafiri.

Meneja wa stendi kuu ya magari ya abiria iliyopo mjini hapa, Dustan Mapunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alisema onyo hilo limetolewa baada ya kupokea malalamiko kuwa wapiga debe wamekuwa na kawaida ya kuwadhalilisha na kuwasumbua abiria jambo ambalo wakati mwingine husababisha mizigo yao kupotea.

Mapunda alisema hatua kali zitachukuliwa kwa kampuni au basi lolote ambalo litaonekana kuleta usumbufu kwa abiria na kwamba lazima wafanyakazi wawe na vitambulisho na orodha yao ipelekwe katika kituo kidogo cha Polisi cha stendi.


“Vitendo hivi vinawanyima uhuru abiria wetu, kwa hiyo ni marufuku abiria kunyang’anywa mizigo, kuvutwa, kutukanwa au kufanyiwa kitendo chochote cha kuwasumbua”, alisema Mapunda.

Pamoja na mambo mengine akizungumzia suala la usafi katika eneo hilo la stendi, alisisitiza kuwa kila basi liwe na chombo cha kuhifadhia takataka huku akiwataka abiria kutotupa taka ovyo kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.

Aidha Meneja huyo alikemea vitendo vya kuuza vyakula ndani ya eneo la stendi bila mpangilio ambapo aliwat aka mama malishe kufuata taratibu zilizowekwa kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.


Hata hivyo aliwataka waendesha pikipiki, maarufu kwa jina la Yeboyebo kutoingia na pikipiki ndani ya stendi hiyo badala yake watapangiwa eneo maalumu la kupaki pikipiki zao wakati wanasubiri abiria wa kuwabeba.


No comments: