Sunday, November 9, 2014

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA APOKELEWA KWA MABANGO, VIGOGO WILAYA YA MBINGA MATUMBO JOTO

Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Hussein Mwinyi akisalimiana na wana CCM wakati alipowasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho wilayani Mbinga.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho akisistiza jambo ndani ya kikao cha Halmashauri kuu ya mkoa wa Ruvuma kilichofanyika ukumbi wa Jumba la maendeleo wilayani Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Dokta Hussein Mwinyi, ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, amepokelewa kwa mabango wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yakiwatuhumu baadhi ya vigogo wa ngazi ya juu wilayani humo kufuatia mgogoro mkubwa uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na Afisa elimu wa shule za msingi wa wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi ambao ni wanachama wa CCM, ndio walioshika mabango hayo ambayo yalikuwa na ujumbe uliosomeka kuwa; Afisa elimu wetu anaonewa, Mkurugenzi wa halmashauri hatumtaki ondoka nae, Afisa usalama wa taifa (DSO) hatufai ondoka nae, Hawa ndio wanaoimaliza CCM Mbinga, Wananchi wanaichukia CCM kupitia hawa watu na mwishoni kabisa yalikuwa yakimalizia kwa kauli ya Tafadhali sikiliza vilio vyetu wanambinga.

Hayo yote yalitokea wakati Waziri Mwinyi anawasili katika viwanja vya makao makuu ya Ofisi za Chama cha mapinduzi wilayani Mbinga, leo majira ya saa 5: 30 ambapo wanachama hao walionekana kujawa jazba huku wakipinga mgogoro huo ambao unaendelea kufukuta mpaka sasa wilayani humo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanachama hao ambao walionekana wameshika mabango hayo ambayo yalisheheni ujumbe huo wa kuwakataa viongozi hao wa wilaya hiyo, ghafla alijitokeza Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani hapa Joseph Mkirikiti ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akiwa ameongozana na Afisa usalama wa taifa wa wilaya ya Mbinga (Jina tunalo) walikwenda mbele ya mabango hayo na kuyanyang’anya na baadae wanachama hao walikamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, zinaarifu kuwa wanachama hao walikuwa wakihojiwa na kuchukuliwa maelezo kituoni hapo na kuambiwa kesho Novemba 10 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi wakaripoti tena.

Aidha wanachama hao wanatuhumiwa kuwa ndio waliohusika kusambaza waraka uliosheheni tuhuma mbalimbali, ambazo zinamtuhumu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga kuwa anamuonea Afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo Daud Mathias Mkali.


Waziri akabidhiwa waraka wenye taarifa ya kusimamishwa kazi Afisa elimu msingi wilaya Mbinga:

Wakati Waziri Mwinyi anawasili katika viwanja vya Chama cha mapinduzi wilaya ya Mbinga, baadhi ya wanachama wa chama hicho Monica Msuku na Salima Mkeso walimkabidhi taarifa ya maandishi juu ya kusimamishwa kazi Afisa elimu wa wilaya hiyo Bw. Mkali ambayo nakala yake tunayo, ambapo imefafanua dhahiri kuwa afisa elimu huyo anaonewa.

Moja kati ya sehemu ya taarifa hiyo ambayo inakurasa nane, inaeleza kuwa tuhuma anazotuhumiwa afisa elimu huyo, mazingira ya vikao vyote vilivyoshughulikiwa dhidi yake na mwisho kwenye kikao cha baraza la madiwani cha tarehe Oktoba 27 mwaka huu yaliandaliwa na kutumika kama njia na silaha pekee ya kumuazimia, kumwajibisha na kumchukulia hatua zaidi, sambamba na madiwani kumkataa.

Vilevile Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, katika kipindi chote cha mwaka mmoja alichofanya naye kazi Afisa elimu huyo, hajawahi kuitwa au kuonya kuhusiana na masuala ya kazi, hata pamoja na kutokuonya na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu amekuwa akikumbana na changamoto zinazohusiana na mambo ya fedha, ambayo ameyafanya Mkurugenzi wa wilaya ya Mbinga kama ifuatavyo;

Na nukuu;

Mkurugenzi mtendaji katika taarifa hiyo anadaiwa, kupunguza bakaa la fedha za idara ya elimu msingi, ambapo wakati wa Juni 30 mwaka 2013 idara hiyo ilibakiwa na fedha shilingi milioni 127,110,696.90 lakini siku iliyofuata Julai 1 mwaka 2013 aliigawia idara ya elimu msingi bakaa la shilingi milioni 73,000,000. Afisa elimu msingi alipojaribu kufuatilia kwa kuwasiliana na Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo alikuwa mkali na kumfokea.

Jambo lingine ni kwamba Mkurugenzi huyo anadaiwa, kutopeleka fedha za Capitation kwa wakati kadri ya miongozo ya MMEM na fedha kukaa zaidi ya mwaka bila kupelekwa mashuleni, na alipojaribu Afisa elimu kuandika barua za kukumbusha ili kusisitiza fedha ziende kwa wakati pia alifokewa na kujengewa uadui ambao unaendelea hadi sasa.

Aidha fedha za Capitation za mwaka 2012/2013 jumla ya shilingi milioni 54,725,000 hazijapelekwa shuleni mpaka sasa, pamoja na Wakaguzi wa mkoa kukagua na kutoa hoja hiyo Novemba 11 mwaka 2013 pamoja na kikao cha kamati ya mipango na fedha cha Julai 10 mwaka huu kupitia hoja hiyo na kuweka msisitizo, pamoja na msisitizo wa kikao cha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania cha Marchi 1 mwaka huu lakini hadi Oktoba 16 mwaka huu fedha hizo za Capitation zilikuwa hazijapelekwa mashuleni.

Idara iliandaa fedha za kuwalipa walimu waliofundisha muda wa ziada wakati wa likizo ya Desemba 2013 lakini fedha hizo, baada ya kutoka zilichukuliwa na Mkurugenzi mtendaji wa wilaya kwa maelezo ya kuwa anaziazima lakini hadi leo hii walimu hawajalipwa.

Kipindi cha mwezi Juni 2014 Afisa elimu aliitwa nyumbani kwake Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga, na kuagizwa awasiliane na uongozi wa Waratibu elimu kata wampatie fedha shilingi milioni 10,000,000 kutoka katika mfuko wa umoja wa waratibu hao (UWEKAMBI), agizo ambalo afisa elimu alishindwa kulitekeleza na badala yake kujengea uhasama uliopelekea kuanza kuwasakama waratibu elimu kata, na kumhusisha afisa elimu kama kiongozi wa idara na kudai kuwa huo umoja wa kazi wa waratibu elimu kata ni NGO yake.

Idara ya elimu ya msingi kwa muda mrefu maombi na madokezo ya fedha yalikuwa hayapitishwi na kuidhinishwa kwa malipo, hali iliyosababisha hata gari la idara hiyo kufanyiwa matengenezo kwa fedha za mfukoni ikiwa pamoja na kununua matairi na betri.

Mwisho wa taarifa hiyo unaeleza kuwa hali hiyo imedumu mpaka siku Afisa elimu msingi anasimamishwa kazi, ndipo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga alikwenda idara ya elimu kuwataka walete madokezo yao yapitishwe na yalipitishwa kwa siku moja.

Yaliyojiri katika kikao:

Pamoja na mambo mengine Waziri Mwinyi ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Ruvuma, wakati anawasili katika kikao alichoandaliwa kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ili aweze kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya mkoa huo, mapya yaliibuka katika mkutano huo ambapo Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa Oddo Mwisho ndiye aliyeibua hasira kutoka kwa wanachama wengine,  juu ya mgogoro huo unaoendelea kufukuta kati ya afisa huyo wa elimu msingi na mkurugenzi wake mtendaji huku akimtaka Waziri huyo kuingilia kati ili kuweza kunusuru maendeleo ya elimu wilayani humo.

“Suala hili la mgogoro kati ya mkurugenzi huyu na afisa elimu, mimi nasema endapo kama litaendelea nipo tayari kulifikisha kwa viongozi wa ngazi ya juu ili lifanyiwe kazi, hatutaweza kuvumilia migogoro ya watendaji wa serikali inaendelea katika wilaya hii, hapa anayeumia ni mwananchi wa kawaida”, alisema Mwisho.

Mwenyekiti wa CCM wilaya Mbinga awa Mbogo:

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Mbinga Christantus Mbunda, aligeuka kuwa mbogo katika kikao hicho huku akiwanyoshea kidole viongozi wa ngazi ya juu wa wilaya  hiyo, akisema kwamba ndio wanaolea na kushabikia mgogoro huo uendelee kukua huku wakiendelea kukaa maofisini bila kuchukua hatua madhubuti.

Mbunda alisema ofisini kwake ameletewa barua nyingi za malalamiko juu ya tatizo hilo, lakini akiwa katika vikao husika na viongozi wenzake wa wilaya hiyo wanaonekana wakimpinga na kutoonesha njia ya kufanya utatuzi.

Alisema kwamba, ili kuweza kufanikisha suala hilo liweze kufikia hatua ya kwisha kwa amani ni vyema ngazi ya chama mkoa na taifa kwa ujumla, wakaingilia kati ikiwemo hata kuwajibisha watendaji ambao wanaonekana kulea mambo ambayo yanakipeleka chama kubaya na wilaya hiyo.

“Mheshimiwa Waziri nipo tayari kusulubiwa katika hili, nitasema ukweli daima ndani ya chama sitaki unafiki, hapa Mbinga kumechafuka Mkurugenzi sasa amefikia hatua ya hata kuwahamisha waratibu elimu kata bila kufuata taratibu kwa sababu tu ya mgogoro huu ambao anauendekeza na watu wake anaowajua yeye,

“Sisi kama chama tukiona kuna mtendaji wa serikali ana dalili tosha ya kutaka kukiharibu chama kama ilivyo kwa mgogoro huu, hatutakuwa na msamaha naye haki ya mtu haipotei ila inacheleweshwa,

“Kutunishiana misuli hakutakiwi, kwa wale watendaji wanaotupuuza tusimame kidete kama viongozi wa chama kupinga jambo hili kwa nguvu kubwa”, alisema Mbunda.

Aliongeza kuwa watendaji wa serikali wasipokuwa na ushirikiano kati ya chama tawala kilichopo madarakani maendeleo kwa wananchi hayatakuwepo, ni vyema viongozi wa namna hiyo wakawajibishwa mapema kwa manufaa ya umma ili wasilipeleke taifa kubaya kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa anena:

Akijibu hoja juu ya mgogoro huo uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji na Afisa elimu wa wilaya ya Mbinga, Waziri Mwinyi alisikitishwa na kitendo hicho na kusema haki itendeke asionewe mtu na kama viongozi katika ngazi ya wilaya na mkoa watashindwa kulimaliza jambo hili, ameagiza liletwe ngazi ya taifa na yupo tayari kulifanyia kazi.


Mwinyi alisema anashangazwa na viongozi wa wilaya hiyo kushindwa kumaliza mgogoro huo kwa wakati badala yake unaendelea kudumu kwa muda mrefu, hadi unafikia hatua ya kuwachukiza wananchi wa Mbinga na kuhatarisha sekta ya elimu msingi kurudi nyuma wilayani humo, wakati wilaya hiyo hivi sasa inang’ara kitaifa kufanya vizuri katika elimu.

No comments: