Monday, November 10, 2014

OFISI YA MKAGUZI WA NDANI MBINGA KUNA MATATIZO NI VYEMA YAKAFANYIWA KAZI

Rais Jakaya Kikwete, wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


OFISI ya Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imeshushiwa shutuma nzito kwamba inashindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa, badala yake inatoa taarifa zenye mapungufu na kuleta migogoro isiyokuwa na tija, mtandao huu umeambiwa.

Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo Laston Kilembe, ndiye anayeshushiwa shutuma hizo na baadhi ya madiwani wa wilaya hiyo, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti.

Walisema hata Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alimuagiza mkaguzi huyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Julai 26 mwaka huu mjini hapa, kwamba ahakikishe anatoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.


Sambamba na hilo Mkuu huyo wa mkoa aliwataka hata watendaji wa serikali katika halmashauri hiyo, kutoingilia utendaji kazi wa ofisi ya mkaguzi huyo huku akisema kuwa ni ofisi ambayo ipo huru na inafanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Walifafanua kuwa ofisi ya mkaguzi wa ndani katika halmashauri yoyote hapa nchini, ni idara kamilifu ambayo ipo huru na haipaswi kuingiliwa na mtu.

Walibainisha mambo hayo yote yanatokana na madiwani kupinga taarifa yake ya ukaguzi kwamba ina mapungufu, juu ya tuhuma anazotuhumiwa Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga kwamba ni mwizi wa mafuta na fedha za michango ya wananchi.

Diwani wa kata ya Litembo Altho Hyera alisema anamshangaa Bw. Kilembe kuwasilisha  tuhuma hizo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni, huku akijua fika taarifa yake haikukamilika na ina mapungufu makubwa kutokana na kufanya ukaguzi usiokidhi matakwa husika.

Hyera alisema taarifa hiyo ambayo madiwani waligawiwa katika kikao hicho alipomaliza kuisoma mbele ya baraza, ghafla walishangaa kumuona Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hussein Ngaga anasimama na kusema taarifa hiyo bado haijakamilika inafanyiwa kazi itatolewa majibu katika kikao kingine kijacho cha madiwani.

Alisema baadae Mkurugenzi huyo aliamrisha taarifa zote zilizokuwa mikononi mwa madiwani zikusanywe watapewa tena katika kikao kijacho, jambo ambalo wengi wao walikuwa wakihoji kama taarifa hiyo ilikuwa na mapungufu na haijakamilika kwa nini ililetwa mbele ya baraza hilo na kuwasilishwa?.

Kufuatia hali hiyo ndipo walipoelekeza hasira zao kwa mkaguzi wa ndani kwamba anashindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi ipasavyo, badala yake anatengeneza majungu yenye kuleta mifarakano kati ya madiwani na watendaji wa serikali katika halmashauri hiyo.

Waandishi wa habari walipokwenda ofisini kwa mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Laston Kilembe, kumtaka atolee ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alikataa kuzungumzia lolote huku akisema mpaka apate kibali kutoka kwa mkurugenzi wake.

“Siwezi kuzungumza nanyi mpaka mpate kibali kutoka kwa mkurugenzi, fuateni taratibu mkurugenzi mimi ni bosi wangu, hata kama ofisi yangu inafanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yoyote lakini siwezi kuzungumza lolote mpaka nipate kibali kutoka kwake”, alisema Kilembe.

No comments: