Monday, November 28, 2016

CHAWATA MBINGA YATOA MSAADA WA BAISKELI MAALUM KWA MWANAFUNZI WA SEKONDARI RUANDA

Damian Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Ruanda mara baada ya kukabidhiwa baiskeli maalum ya kutembelea.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimetoa msaada wa baiskeli maalum ya kutembelea mlemavu Damian Kapinga (22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya sekondari Ruanda wilayani humo yenye thamani ya shilingi milioni moja.

Akikabidhi msaada huo shuleni hapo mbele ya Mkuu wa shule Stephano Ndomba na Diwani wa viti maalum tarafa ya Namswea Immaculatha Mapunda, Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa Martin Mbawala alisema kuwa baiskeli hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na chama, kutoka kwa wasamaria wema.

Mbawala alisema kuwa chama kimefanya jitihada ya kutafuta baiskeli hiyo kutokana na taabu alizokuwa akizipata mtoto huyo kutambaa kwa mikono na magoti wakati wa kwenda shule kuhudhuria masomo yake, hivyo kiliona kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kumrahisishia asiendelee kupata adha hiyo.

“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia uweze kutembea na kuhudhuria masomo yako vizuri, nawaomba viongozi wa kata hii ya Ruanda muendelee kumtunza mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana matatizo ya ulemavu”, alisisitiza Mbawala.

SERIKALI YAOMBWA KUINUSURU HOSPITALI YA MISHENI MBESA TUNDURU

Na Kassian Nyandindi,        
Tunduru.

HOSPITALI kongwe ya Misheni Mbesa ambayo inamilikiwa na Kanisa la Bibilia Tanzania wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ipo katika hali mbaya yenye kuhatarisha kufungwa wakati wowote kuanzia sasa kutokana na Madaktari kutoka nje ya nchi ambao walikuwa ni tegemeo kubwa katika kuendesha hospitali hiyo kuanza kufunga virago kurejea makwao, baada ya mikataba yao ya kufanya kazi kwisha.

Hospitali ya Misheni Mbesa.
Katibu tawala wa hospitali hiyo, Dkt. John Mwaya alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya hospitali yake kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera ambaye alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea maendeleo mbalimbali.

Dkt. Mwaya alibainisha kuwa changamoto kubwa inayotishia kufa kwa hospitali yake ni kuwepo kwa upungufu wa Madaktari wenye taaluma na wauguzi walio somea fani hiyo ili kuweza kutosheleza ikama husika.

Sunday, November 27, 2016

MBUNGE WA TUNDURU KUSINI AMWAGA NEEMA KWA WANANCHI WAKE


Na Julius Konala,     
Tunduru.

MBUNGE wa Jimbo la Tunduru kusini mkoani Ruvuma, Daimu Mpakate ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100 ili viweze kutumiwa na wananchi wake jimboni humo, kwa ajili ya kuwaletea maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Daimu Mpakate.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo alisema kuwa miongoni mwa misaada iliyotolewa ni mashine nane za kusaga nafaka zenye thamani ya shilingi milioni 16, vitabu vya kiada na ziada kwa shule za sekondari vyenye thamani ya shilingi milioni 32, mashine za kushonea nguo (vyerehani) nane vyenye thamani ya shilingi milioni 2, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 2 kwa ajili ya kugharimia kushona sare za shule kwa wanafunzi 120 watakaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.

Mpakate alitoa msaada huo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya serikali ya kijiji cha Mbesa wilayani humo ambapo vifaa hivyo vilitolewa kwa matumizi ya jamii kupitia shule nane za sekondari ambazo ni Nalasi, Mbesa, Mchoteka, Malumba, Ligoma, Lukumbule, Namasakata na Semeni.

HALMASHAURI MANISPAA SONGEA YAVUKA LENGO LA UTOAJI CHANJO


Na Gideon Mwakanosya,          
Songea.

HALMASHAURI Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imevuka lengo la utoaji chanjo kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano na kufikia asilimia 217.5 katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alimweleza mwandishi wetu kuwa katika kutekeleza zoezi hilo la chanjo ya kitaifa kwa kuhakikisha kila mtoto anafikiwa, limeweza kuleta ufanisi mkubwa kwa kukidhi vigezo vya utoaji chanjo ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yale yanayozuiliwa kwa chanjo.

“Manispaa yetu imevuka lengo hili kutokana na watoto na akina mama wajawazito kutoka nje ya halmashauri, kupata huduma katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya”, alisema.

Monday, November 21, 2016

NFRA SONGEA YAONGEZA BEI YA KUNUNUA MAHINDI YA MKULIMA

Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea mkoani Ruvuma, imelazimika kuongeza bei ya kununua mahindi ya wakulima kufuatia kuwepo kwa ushindani mkubwa kutokana na wanunuzi binafsi wengi wao mkoani humo, kununua mahindi kwa bei kubwa kutoka kwa wakulima wanaozalisha zao hilo.

Aidha kufuatia kuwepo kwa ushindani huo, NFRA imeongeza bei ambapo awali walikuwa wakinunua kwa shilingi 350 kwa kilo na kwamba kuanzia Novemba 7 mwaka huu wananunua mahindi kwa shilingi 580 kwa kilo maeneo ya vijijini na shilingi 600 kwa wale wanaoleta katika kituo kikuu cha Ruhuwiko kilichopo mjini hapa.

Kaimu Meneja wa Wakala huyo Kanda ya Songea, Majuto Chabruma alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya zoezi la ununuzi wa mahindi linavyoendelea katika vituo mbalimbali vilivyotengwa katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma.

HALMASHAURI YATENGA MAMILIONI YA FEDHA KUBORESHA ZAO LA KOROSHO NAMTUMBO

Na Muhidin Amri,            
Namtumbo.

KATIKA kuhakikisha kwamba zao la korosho linaboreshwa na kuwa endelevu, halmashauri wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kufufua na kuendeleza zao hilo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Kati ya fedha hizo shilingi milioni 5 zitatumika kununua miche ya zao hilo na shilingi milioni 5 zinazobakia zitatumika kwa ajili ya kununua mbegu za korosho kutoka chuo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara.

Zao la korosho.
Afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilayani Namtumbo, Ally Lugendo aliyataja maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni pamoja na kata ya Magazini, Lusewa, Msisima, Ligera, Lisimonji, Limamu, Likuyu, Mchomoro na Rwinga ambapo mbegu na miche hiyo itasambazwa katika maeneo hayo ambayo yana hali nzuri ya hewa inayostawi vizuri korosho.

Alisema kuwa halmashauri imefikia uamuzi wa kufufua zao la korosho baada ya kuwepo kwa soko la uhakika katika kipindi cha msimu wa mwaka huu ambapo bei imepanda kutoka shilingi 1,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 jambo ambalo halmashauri inaamini kwamba kama wakulima wataamua kuwekeza katika kilimo hicho wataweza kuondokana na umaskini katika familia zao.

Sunday, November 20, 2016

WAJASIRIAMALI SONGEA WANUFAIKA NA MIKOPO WASISITIZWA KUITUMIA KWA MALENGO YALIYOKUSUDIWA

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WAJASIRIAMALI waliopo katika vikundi vya wanawake na vijana halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepewa shilingi milioni 20 na halmashauri hiyo ili waweze kuendeleza vikundi vyao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

Fedha hizo walizopewa ni mkopo ambao unalenga kusaidia vikundi 42 vya wajasiariamali hao na sehemu ya mkopo huo watapaswa kurejesha baada ya miezi 12 ambapo kila kikundi kimepewa kuanzia shilingi 800,000 huku vingine vikipewa shilingi 600,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Ofisa habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo alisema kwamba vikundi vilivyopewa fedha hizo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika Manispaa ya Songea.

Tuesday, November 15, 2016

WALIOKAMATWA WAKITOROSHA KAHAWA MBINGA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kassian Nyandindi,                   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba katika tuhuma ambazo zimefikishwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, juu ya suala la utoroshaji wa zao la kahawa ni lazima shauri hilo lifikishwe Mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

Cosmas Nshenye.
Aidha alisema kuwa ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya Watendaji wa serikali kushindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo juu ya namna ya kudhibiti hali hiyo, hatua ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine wafanyabiashara wajanja kutumia mwanya huo kuvunja sheria zilizowekwa na serikali wakiwa na lengo la kukwepa kulipa kodi au ushuru halali kwa mujibu wa sheria.

Nshenye alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia kukamatwa kwa mfanyabiashara, Khatwib Rajabu mkazi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera akidaiwa kushirikiana na wenzake kufanya tukio la utoroshwaji wa kahawa wilayani hapa, bila kufuata taratibu na sheria husika zilizowekwa na serikali.

“Hapa kesi lazima iwepo na kama sio kwa mfanyabiashara aliyehusika kutorosha kahawa basi itabaki kwa watumishi wa serikali waliohusika kutoa kibali hiki, huku wakijiua kwamba wanafanya makosa”, alisisitiza Nshenye.

Saturday, November 12, 2016

HATIMAYE MWILI WA SPIKA MSTAAFU SAMUEL SITTA WAZIKWA URAMBO TABORA

HATIMAYE Novemba 12 mwaka huu yamefanyika mazishi ya Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel John Sitta ambaye alifariki dunia Novemba 7 mwaka huu 2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.


Mazishi hayo yamefanyika Urambo Tabora, kwenye eneo la makaburi ya ukoo wa Sitta ambayo yapo takribani kilometa mbili kutoka nyumbani kwake marehemu Sitta. (Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi….Amen)

CHADEMA WAFUKUZANA UANACHAMA SONGEA FUIME ADAIWA KUKALIA KUTI KAVU

Joseph Fuime akiwa katika majukwaa ya mikutano ya siasa mjini Songea iliyofanyika hivi karibuni.
Na Gideon Mwakanosya,           
Songea.

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimemvua uanachama Joseph Fuime akidaiwa kufanya makosa mbalimbali ikiwemo kukihujumu chama hicho wakati alipokuwa mgombea ubunge kupitia tiketi ya CHADEMA jimbo la Songea mjini, katika uchaguzi mkuu uliopita Oktoba 25 mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake, Katibu wa CHADEMA wilaya ya Songea, Olais Ng`ohison alisema kuwa Fuime amefutwa kwenye orodha ya kuwa mwanachama wa chama hicho, tangu Octoba 23 mwaka huu na kwamba  hivi sasa sio mwanachama tena wa chama hicho.

Alisema kuwa chama hicho kimelazimika kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwajuza wananchi, wadau, wakereketwa pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali baada ya kubaini kwamba watu wengi walikuwa hawafahamu kuondolewa na kufutwa uanachama kwa Fuime.

Friday, November 11, 2016

WAZIRI MKUU AONGOZA BUNGENI KUUAGA MWILI WA MAREHEMU SAMUEL SITTA

Na Waandishi wetu, 
Dodoma.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza mamia ya wabunge, viongozi wa kitaifa na watumishi wa Ofisi ya Bunge kuuaga mwili wa Spika Mstaafu, Samwel Sitta.

Sitta alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 7 mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo Bungeni mjini Dodoma leo Novemba 11 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, mke wa marehemu Sitta, Margareth Sitta, mama wa marehemu Hajat Zuena Fundikila na familia ya marehemu na wabunge wote.

“Nitumie fursa hii pia kukupa pole Mheshimiwa Spika kwa pigo ambalo Bunge lako tukufu imelipata kwa kumpoteza mmoja wa viongozi mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu,

“Msiba uliotupata wa Spika huyu mstaafu wa Bunge la tisa (2005-2010) na Mbunge mstaafu wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora ni mzito”, alisema Majaliwa.

Alisema kuwa Sitta alikuwa ni mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

“Serikali imepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa, historia ya mzee Sitta ni pana sana, tunatambua utumishi wake uliotukuka katika nyadhifa mbalimbali alizozitumikia tutamkumbuka kwa utumishi wake,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Watanzania tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu kila mtu kwa imani yake ili tuweze kufikia japo mema machache aliyoyatenda katika enzi za uhai wake.

Enzi za uhai wake, Marehemu Sitta alibahatika kufanya kazi na marais wa awamu ya nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa mbunge kwa miaka 30.

Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri anayesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (wapili kulia) akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sitta kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016. 

WATEKETEA KWA MOTO WALIPOKUWA PORINI WAKIWINDA

Na Kassian Nyandindi,              
Songea.

WATU wawili ambao ni wakazi wanaoishi katika kijiji cha Mbwambwa kata ya Mpitimbi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia baada ya kuungua moto waliokuwa wameuwasha wakati wakiwa wanawinda porini.

Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Zubery Mwombeji aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Athuman Hashim (16) na Said Liugu (27) wote wakazi wa kijiji hicho.

Mwombeji alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 9 mwaka huu majira ya saa 7 mchana ambapo Hashim na Liugu ambao wamekuwa wakijishughulisha na uwindaji walienda bondeni kwenye kijiji hicho ambako walichoma moto pori walilokuwa wakiwinda, kwa lengo la kutaka kuwaona kwa urahisi wanyama aina ya Ndezi ambao walikuwa wakiwawinda.

Thursday, November 10, 2016

MWILI WA MAREHEMU SAMUEL SITTA WAWASILI JIJINI DAR


Na Mwandishi wetu;

MWILI wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta umewasili jioni hii leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, ukitokea nchini Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.

Mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege, mwili wa Marehemu Sitta umepelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.

MFAHAMU DONALD TRUMP URAIS TAIFA LA MAREKANI KUTOKA CHAMA CHA REPUBLICAN

ALIZALIWA 14 Juni 1946 huko Jamaica Estates, Queens akiwa ni mtoto wa pili kwenye familia ya watoto wanne wa familia ya Mary na Fred Trump na kukulia katika Jiji la New York, Marekani. 

Upande wa baba yake (Fred Trump aliyefariki mwaka 1981), alikuwa mzaliwa wa Ujerumani na mama yake (Mary) ni mzaliwa wa Scottish. 

Trump alianza kusoma katika Chuo Kikuu cha Fordham kilichopo Bronx mwaka 1964, miaka miwili baadaye alihamishiwa katika Shule ya mambo ya fedha na Uchumi ya Wharton iliyopo Chuo Kikuu cha Pennsylvania ambako alihitimu shahada ya kwanza katika masuala ya uchumi mwaka 1968 kabla ya kujiunga na kufanya kazi kwenye kampuni ya familia yake iliyoitwa Elizabeth Trump & Son. 

Mwaka 1971 Trump alikabidhiwa kuongoza makampuni na biashara za baba yake ambapo alipata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi ambayo mpaka sasa ndiye mkurugenzi wake mkuu.

Trump ambaye ni baba wa watoto watano, ni mfanyabiashara mkubwa na bilionea nchini Marekani, pia ni mtayarishaji wa vipindi vya televisheni. 

NSHENYE AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI MBINGA WANAOSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO WAJIONDOE MAPEMA

Na Kassian Nyandindi,                   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya watendaji wa serikali wilayani humo wanaoshindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo hatua ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine, wananchi wazivunje kwa kukataa kutii maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa serikali.
Cosmas Nshenye.

Nshenye alitolea mfano kwa agizo la serikali kuzuia uuzaji na unywaji wa pombe saa za kazi, hata hivyo mamlaka zinazohusika kusimamia hilo kama vile jeshi la Polisi na halmashauri kupitia kitengo chake cha biashara wahusika wamekuwa wakikaa kimya bila kuchukua hatua.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza maafisa biashara wa halmashauri ya wilaya na mji wa Mbinga, kuwakamata na kuwapiga faini au kuwafutia leseni wale wote wanaofanyabiashara ya kuuza pombe saa za kazi.

Alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Nshenye aliwataka pia watumishi wa umma kutimiza wajibu wao ipasavyo pasipo kusubiri kusukumwa  kwani  ni kosa kwa mtumishi wa serikali kushindwa kuleta tija eneo lake la kazi kwani serikali ya awamu ya tano, tangu ilipoingia madarakani imedhamiria kuleta mabadiliko makubwa kwa Watanzania ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na maisha bora kwa wananchi wake kwa kuwapatia huduma zilizokuwa bora.

ASKOFU NDIMBO: WANAUME WANAOKATISHA MASOMO WANAFUNZI WA KIKE WAPEWE ADHABU KALI

Na Mwandishi wetu,          
Mbinga.

ASKOFU wa Kanisa katoliki jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo ameitaka serikali ya awamu ya tano kutokuwa na huruma kwa wanaume ambao wanakatisha masomo ya wanafunzi wa kike waliopo mashuleni kwa kuwapa mimba huku wengine wakidiriki kuwaoa, kwani ni wakati sasa wa kuwachukulia hatua na adhabu kali za kisheria ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Askofu John Ndimbo.
Vilevile alisema kuwa vitendo hivyo licha ya kuwa havimpendezi Mungu, vimekuwa vikikatisha ndoto za watoto wengi wa kike hapa nchini na kurudisha nyuma maendeleo yao sasa umefika wakati wa kutofumbia macho hali hiyo.

Askofu Ndimbo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akizungumza na madiwani, watumishi na baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

POLISI TUNDURU KUWAKAMATA WAPIKA GONGO NA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI

Na Mwandishi wetu,                   
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru Juma Homera, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani hapa kuhakikisha kwamba linawakamata na kuwafikisha Mahakamani baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mbati ambao wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu aina ya gongo.

Pia ametoa siku tatu kwa serikali ya kijiji hicho viongozi wake kwenda ofisini kwake kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kuwepo kwa wanananchi, wanaovunja sheria za nchi hivyo kukwamisha juhudi za serikali katika kupambana na vitendo vya uhalifu ambavyo vinachangia kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Homera alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara ambapo aliwataka wakazi wa kijiji hicho kuwafichua wale wote ambao wamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo kazi ya ufyatuaji tofali 100,000 kwa kila kijiji agizo ambalo lilitolewa na Rais Dkt. John Magufuli.

Tuesday, November 8, 2016

DC TUNDURU AWATAKA WANANCHI KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KWA KUJITUMA KUFANYA KAZI

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akisisitiza jambo katika mikutano yake ya hadhara wilayani hapa hivi karibuni.
Na Muhidin Amri,              
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera amewataka wananchi wa wilaya hiyo kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwa kujikita zaidi katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao badala ya kutumia muda wao mwingi, kupiga porojo za kisiasa ambazo zimeshapita muda wake.

Aidha Homera, amewahimiza kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wakati serikali nayo ikijiandaa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, jambo ambalo litasaidia kuongeza uzalishaji mashambani.

Ametaoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika ziara yake ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji mbalimbali vya kata ya Malumba, Nakapanya, Nandembo na Mpanji wakati akikagua pia zoezi la ufyatuaji tofari kwa kila kijiji wilayani humo.

WANANCHI RUANDA WAKUMBWA NA MAAFA YA KUEZULIWA NYUMBA ZAO RC RUVUMA ASIKITISHWA OFISI YAKE KUTOPEWA TAARIFA KWA WAKATI

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

JUMLA ya Kaya saba zenye wakazi zaidi ya 40 waishio katika kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamekosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo mkali.

Tukio hilo lilitokea Novemba Mosi mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika kata hiyo, huku wengine baadhi yao nyumba zao zikiwa zimenusurika kubomolewa baada ya kuezuliwa na upepo huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema kuwa jumla ya nyumba 32 za wananchi ziliezuliwa na upepo huo.

Sunday, November 6, 2016

DC MBINGA APIGA MARUFUKU UNYWAJI POMBE SAA ZA KAZI AMTAKA AFISA BIASHARA KUNYANG'ANYA LESENI KWA WANAOKAIDI

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amepiga marufuku unywaji pombe saa za kazi na kumtaka Afisa biashara mwenye dhamana ya kusimamia suala hilo, ahakikishe kwamba anadhibiti hali hiyo ili isiweze kuendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Nshenye alitoa rai hiyo juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo aliagiza pia kuwashughulikia wale wote ambao wanauza pombe saa za kazi asubuhi.

“Leseni za biashara naagiza zinyang’anywe kwa wale wanaouza pombe saa za asubuhi, haiwezekani watu wanaacha kufanya kazi badala yake utaona wanakwenda kwenye baa na kunywa pombe, pombe zote zianze kunyweka kuanzia saa tisa jioni”, alisisitiza Nshenye.

Aliongeza kuwa kwa wale watumishi ambao watashindwa kusimamia majukumu ya kazi zao ipasavyo, wajiandae kuacha kazi au wajiondoe mapema wenyewe kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.

MBINGA WAONYWA TABIA YA KUWAFUNGIA WATOTO WENYE ULEMAVU NDANI YA NYUMBA ZAO

Baadhi ya watoto wenye ulemavu (Albino) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa halmashauri ya mji wa Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,               
Mbinga.

WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa kuacha tabia ya kuwafungia ndani ya nyumba zao watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali badala yake wajenge mazoea ya kuwafichua watu wenye tabia ya kuwaficha watoto hao, ili waweze kupata haki zao za msingi.

Aidha wameshauriwa kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye walemavu ikiwemo unyanyasaji, ubaguzi na kwamba wanapaswa kujenga mazoea ya kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia ipasavyo kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana matatizo ya viungo.

Diwani wa viti maalumu kata ya Ruanda, Imakulatha Mapunda alisema hayo juzi alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya sheria ya watu wenye ulemavu, yaliyofanyika katika kata hiyo wilaya ya Mbinga mkoani hapa ambayo yalifadhiliwa na shirika lisilokuwa la serikali la The Foundation for Civil Society.

SERIKALI: MARUFUKU UPIGAJI PICHA KWA WAGONJWA WODINI



Na Muhidin Amri,         
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma, imepiga marufuku upigaji picha kwa wagonjwa wanaolazwa wodini au katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika mkoa huo.

Onyo hilo limetolewa hivi karibuni mjini Songea na Mganga mkuu wa mkoa huo, Dkt. Damas Kayera kwa niaba ya Katibu tawala wa mkoa huo, Hassan Bendeyeko.

Dkt. Damas Kayera.
“Kuanzia sasa  ni marufuku vitendo vya upigaji picha wodini kwa kutumia kamera au vifaa vyovyote vyenye uwezo wa  kupiga picha kama vile simu za mkononi", alisema Dkt. Kayera.

Alisema kuwa wamepiga marufuku kutokana na kile walichobaini kuwa vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa huo, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi kupiga picha wodini pale wanapokuja kuwajulia hali ndugu zao waliolazwa bila kibali maalumu.

Dkt. Kayera alisema kuwa vitendo hivyo vinafanywa ama kwa lengo zuri la kuwajulisha jamaa zao hali ya mgonjwa wao au kwa malengo ambayo sio mazuri ambapo baadhi ya picha zimekuwa zikioneshwa kwenye mitandao ya kijamii zikiwa na ujumbe wa kupotosha.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto katika barua yake kwa makatibu tawala wa mikoa Tanzania bara, inaeleza kuwa Wizara imetoa tamko la kukataza kupiga picha wodini kwa kuwa inasimamia viwango na miiko ya utoaji huduma za afya.

Saturday, November 5, 2016

TUNDURU WAANZISHA OPARESHENI MAALUM YA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MAJENGO

Na Muhidin Amri,       
Tunduru.

WILAYA ya Tunduru  mkoani Ruvuma, imeanza Operesheni maalum ya kukabiliana na upungufu wa majengo ya umma ambapo hivi sasa ufyatuaji wa tofari 100,000 kwa kila kijiji unafanyika,  ili kuweza kupata matofari ya kujengea majengo ya shule kama vile madarasa, nyumba za walimu, zahanati na vyoo.

Akiwa katika hafla ya kukabidhi matofari 7,642,816 kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge katika vijiji vya Ligoma na Makoteni, Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema kuwa, baada ya kubaini  wilaya yake ina upungufu mkubwa wa majengo hayo ya umma wameamua kuanzisha operesheni hiyo ili kuweza kufikia malengo husika.

Homera alimweleza Dkt. Mahenge kuwa matofari hayo ni ya awali tu na kwamba katika baadhi ya vijiji wananchi wanaendelea na kazi hiyo, ambapo vijiji vingine wilayani hapa vipo katika hatua ya kuchoma tofari hizo na kwamba zoezi hilo litakapokamilika wanatarajia kuwa na tofari 16,700,000.

MCHOMORO NAMTUMBO WAPEWA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI ZAHANATI

Na Mwandishi wetu,           
Namtumbo.

WANANCHI wa kijiji cha Mchomoro wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wamepata msaada wa vifaa vya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho kutoka kwa Kampuni inayotarajia kuchimba madini aina ya Uranium, Mantra Tanzania wilayani humo vyenye thamani ya shilingi milioni 16,329,000. 

Vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo ilikabidhi ikiwa ni mchango wake katika kuungana na wananchi wa kijiji hicho, kwa lengo la kukamilisha ujenzi wake ili uweze kukamilika kwa wakati husika uliopangwa.

Ofisa habari wa Kampuni hiyo, Khadija Pallangyo ndiye aliyekabidhi vifaa vya ujenzi kwa uongozi wa kijiji cha Mchomoro ambapo alitoa msaada wa bati 425, saruji mifuko 400, nondo 51, misumari na waya kilo 40, boriti 10 na mbao 20.

Friday, November 4, 2016

WATATU WASHIKILIWA POLISI WAKIDAIWA KUTOA KIPIGO NA KUSABABISHA KIFO

Na Kassian Nyandindi,            
Songea.

WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma ya kuwashushia kipigo kikali watu wawili sehemu mbalimbali za miili yao, wakituhumiwa kuiba kwenye nyumba ya kulala wageni ya Jordan River iliyopo mtaa wa Majengo, Manispaa ya Songea mkoani hapa na kumsababishia kifo Anold James mkazi wa Njombe mjini mkoani Njombe.

Zubery Mwombeji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake, Kamanda  wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu majira ya saa 12:40 asubuhi kwenye maeneo ya nyumba hiyo ya kulala wageni mjini humo.

Mwombeji alifafanua kuwa inadaiwa siku moja kabla ya tukio hilo kutokea watu wawili Anold James (25), James Exavery (18) wote wakazi wa Njombe walifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kuomba chumba cha kulala na kwamba kwenye kitabu cha wageni aliandikishwa mtu mmoja tu ambaye ni, Anold James kisha baadaye James Exavery aliondoka akabaki Anold.

Alisema kuwa baadaye ilipofika majira ya saa za usiku kwenye chumba hicho alichokuwa amelala Anold, kulisikika sauti kuwa kuna watu wengi ndipo Meneja wa nyumba hiyo ya wageni Barnaba Said (22) alilazimika kwenda kuwachungulia ambapo aliona wamekaa kwenye chumba hicho, huku wakinywa pombe na baada ya muda mchache aligundua kuwa kunamali imeibiwa.

Tuesday, November 1, 2016

MADIWANI MBINGA WALALAMIKIA TATIZO LA UPUNGUFU WA MADAWA KATIKA VITUO VYA AFYA



Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikia kuwepo kwa tatizo kubwa la upungufu wa madawa na vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo wilayani humo, jambo ambalo linawafanya wagonjwa wengi washindwe kupatiwa matibabu.

Baadhi yao walisema kuwa licha ya kusikia matangazo kupitia vyombo vya habari kutoka kwa Waziri mwenye dhamana kwamba hakuna tatizo la upungufu wa madawa katika hospitali na vituo hivyo vya afya hapa nchini, hali hiyo imekuwa kinyume ndani ya wilaya hiyo ambapo maeneo mengi wagonjwa wanashindwa kupatiwa matibabu kutokana na kukosekana kwa madawa hayo.

Walifafanua kuwa hata kwa upande wa wanachama wa Mfuko wa bima ya afya (CHF) wengi wao hawapatiwi matibabu ipasavyo kutokana na sehemu ambako wanatolea huduma za afya kutokuwepo kwa madawa na vifaa tiba, jambo ambalo Madiwani katika kata zao wanashindwa kuendelea kuhamasisha wananchi wao waendelee kuchangia mfuko huo.

JESHI LA POLISI RUVUMA LINAWASAKA MAJAMBAZI WALIOPORA MILIONI 15 ZA MFANYABIASHARA KIGONSERA MBINGA



Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linawasaka watu watano wanaodaiwa kuwa ni majambazi ambao walivamia duka la Mfanyabiashara mmoja anayefahamika kwa jina la Msafiri Tullo (40) mkazi wa mji mdogo wa Kigonsera wilayani Mbinga mkoani humo na kumpora fedha taslimu za mauzo shillingi milioni 15,250,000 pamoja na simu mbili za kiganjani aina ya Tecno, zenye thamani ya shilingi 110,000 na kutokomea kusikojulikana.
Zubery Mwombeji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1:30 jioni katika mji huo wa kigonsera.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo palitokea kundi la watu watano huku wakiwa na silaha za jadi ambazo walikuwa wameshika mkononi, ambapo walipowasili dukani hapo walianza kumshambulia Msafiri kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kufanikiwa kumpora fedha hizo huku wakimjeruhi sikio lake la upande wa kushoto na muuzaji wake wa duka hilo, Melkion Nchimbi (18).