Monday, November 21, 2016

HALMASHAURI YATENGA MAMILIONI YA FEDHA KUBORESHA ZAO LA KOROSHO NAMTUMBO

Na Muhidin Amri,            
Namtumbo.

KATIKA kuhakikisha kwamba zao la korosho linaboreshwa na kuwa endelevu, halmashauri wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kufufua na kuendeleza zao hilo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Kati ya fedha hizo shilingi milioni 5 zitatumika kununua miche ya zao hilo na shilingi milioni 5 zinazobakia zitatumika kwa ajili ya kununua mbegu za korosho kutoka chuo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara.

Zao la korosho.
Afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilayani Namtumbo, Ally Lugendo aliyataja maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni pamoja na kata ya Magazini, Lusewa, Msisima, Ligera, Lisimonji, Limamu, Likuyu, Mchomoro na Rwinga ambapo mbegu na miche hiyo itasambazwa katika maeneo hayo ambayo yana hali nzuri ya hewa inayostawi vizuri korosho.

Alisema kuwa halmashauri imefikia uamuzi wa kufufua zao la korosho baada ya kuwepo kwa soko la uhakika katika kipindi cha msimu wa mwaka huu ambapo bei imepanda kutoka shilingi 1,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 jambo ambalo halmashauri inaamini kwamba kama wakulima wataamua kuwekeza katika kilimo hicho wataweza kuondokana na umaskini katika familia zao.

Lugendo alisema kufufuliwa kwa zao la korosho na hata mazao mengine ambayo yalisahaulika kwa muda mrefu ni mkakati wa halmashauri  kuhakikisha wakulima wanakuwa na mazao mengi ya biashara ambayo   halmashuari inayaona kama vyanzo mbadala ya vya mapato  hasa ikizingatia kuwa asilimia 90 ya wakazi wake wanategemea kilimo kama njia kuu ya uchumi.

Katika msimu wa mwaka 2015/2016 halmashauri ilianza pia na mpango wa kulima zao la kahawa na kununua miche 16,668 ambayo tayari imesambazwa kwa wakulima msimu wa mwaka huu na miche 33,330 imeongeza kutoka chuo cha utafiti wa zao la kahawa TaCRI Ugano, kilichopo wilayani Mbinga mkoani humo.

Lugendo alizitaja kata zenye hali nzuri ya hewa inayofaa kwa kilimo cha kahawa ni pamoja na kata ya Likuyu, Litola, Mgombasi, Namabengo, Msindo na Namtumbo ambazo hali yake ya hewa ni baridi tofauti na ilivyo kwa maeneo mengine.

Afisa ardhi na maliasili wa wilaya ya Namtumbo, Mauruce Hyera alisema kuwa, halmashauri imetenga imetenga kilometa za mraba 1,000 ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji na makazi.

Hyera aliongeza kuwa bado wilaya hiyo ina eneo la kilometa za mraba 5,791 hazijatumika na kwamba zinahitaji wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza kwa ajili ya shughuli za kilimo.

“Sisi kama halmashauri tayari kuna maeneo tumeyatenga kwa ajili ya shughuli za kilimo, idara ya ardhi ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kulingana na mwekezaji husika atahitaji kuzalisha zao gani”, alisema.

Pia Hyera  alibainisha kuwa mbali na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hizo vilevile wanaendelea kuuza maeneo mengine kwa ajili ya viwanja vya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, ambapo viwanja zaidi ya 742.

No comments: