Sunday, November 6, 2016

SERIKALI: MARUFUKU UPIGAJI PICHA KWA WAGONJWA WODINI



Na Muhidin Amri,         
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma, imepiga marufuku upigaji picha kwa wagonjwa wanaolazwa wodini au katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika mkoa huo.

Onyo hilo limetolewa hivi karibuni mjini Songea na Mganga mkuu wa mkoa huo, Dkt. Damas Kayera kwa niaba ya Katibu tawala wa mkoa huo, Hassan Bendeyeko.

Dkt. Damas Kayera.
“Kuanzia sasa  ni marufuku vitendo vya upigaji picha wodini kwa kutumia kamera au vifaa vyovyote vyenye uwezo wa  kupiga picha kama vile simu za mkononi", alisema Dkt. Kayera.

Alisema kuwa wamepiga marufuku kutokana na kile walichobaini kuwa vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa huo, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi kupiga picha wodini pale wanapokuja kuwajulia hali ndugu zao waliolazwa bila kibali maalumu.

Dkt. Kayera alisema kuwa vitendo hivyo vinafanywa ama kwa lengo zuri la kuwajulisha jamaa zao hali ya mgonjwa wao au kwa malengo ambayo sio mazuri ambapo baadhi ya picha zimekuwa zikioneshwa kwenye mitandao ya kijamii zikiwa na ujumbe wa kupotosha.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto katika barua yake kwa makatibu tawala wa mikoa Tanzania bara, inaeleza kuwa Wizara imetoa tamko la kukataza kupiga picha wodini kwa kuwa inasimamia viwango na miiko ya utoaji huduma za afya.


Waganga wakuu wa mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wanatakiwa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kwamba wananchi wanatakiwa kuelimishwa umuhimu wa kuwasilisha malalamiko yao  pale inapotokea ukiukwaji wowote katika utoaji wa huduma za afya.

Katika hatua nyingine Manispaa ya Songera nayo imeanza kutekeleza agizo la kupiga marufuku upigaji picha wodini kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Manispaa hiyo.

Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa tayari Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo ametoa maagizo kwa Mganga mkuu wa Manispaa ya Songea kuhakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa kwa vitendo katika hospitali na vituo vya afya.

No comments: