Friday, November 11, 2016

WATEKETEA KWA MOTO WALIPOKUWA PORINI WAKIWINDA

Na Kassian Nyandindi,              
Songea.

WATU wawili ambao ni wakazi wanaoishi katika kijiji cha Mbwambwa kata ya Mpitimbi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia baada ya kuungua moto waliokuwa wameuwasha wakati wakiwa wanawinda porini.

Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Zubery Mwombeji aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Athuman Hashim (16) na Said Liugu (27) wote wakazi wa kijiji hicho.

Mwombeji alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 9 mwaka huu majira ya saa 7 mchana ambapo Hashim na Liugu ambao wamekuwa wakijishughulisha na uwindaji walienda bondeni kwenye kijiji hicho ambako walichoma moto pori walilokuwa wakiwinda, kwa lengo la kutaka kuwaona kwa urahisi wanyama aina ya Ndezi ambao walikuwa wakiwawinda.


Alibainisha kuwa wawindaji hao baada ya kuwasha moto huo ambao baadaye ulionekana kuwashinda, uliwaka sehemu zote ukiwa umewazunguka na kusababisha washindwe mahali pa kukimbilia kwa sababu hata maeneo ya njia ya kurudia wao, moto ulikuwa umewazingira na kusababisha washindwe kujiokoa hadi mauti yalipowakuta.

Vilevile alieleza kuwa watu waliokuwa jirani na eneo hilo walipoona moto mkubwa ukisambaa hovyo walikwenda kwenye eneo la tukio kusaidia namna ya kuuzima lakini ilishindikana na baadaye uongozi wa serikali ya kijiji hicho, kwa kushirikiana na wananchi walipokwenda kwenye eneo la tukio hilo kwa lengo la kuuzima pia nao walishindwa.

Alisema kuwa baadaye moto ulipopungua ndipo waliiona miili ya watu wawili wakiwa wameungua moto ambao baadaye walifahamika kuwa ni  Hashim na Liugu ambao walikuwa wakijishughulisha na kazi hiyo ya uwindaji.

Kadhalika Polisi walipopewa taarifa kuhusiana na tukio hilo, waliwasili katika eneo la tukio huku wakiwa wameongozana na mganga kutoka kituo cha afya Mpitimbi ambaye alithibitisha kuwa watu hao tayari walikuwa wamekufa kutokana na kuungua moto.

Pia ndugu wa marehemu hao waliwasili nao kwa ajili ya kuchukua miili hiyo kwa ajili ya taratibu za mazishi.


Hata hivyo katika tukio jingine jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kuwakamata watu wawili Yassin Yassin (44) mkazi wa kijiji cha Mchomoro  na Mussa Sandari (70) mkazi wa kijiji cha Ligela  wilayani Namtumbo mkoani hapa, wakiwa na misokoto ya bhangi gramu 250 na miche ya bhangi 99 iliyokuwa imepandwa katikati ya shamba la mahindi lililopo kwenye hifadhi ya wanyama ya Mbalanga wilayani humo.

No comments: