Monday, November 28, 2016

CHAWATA MBINGA YATOA MSAADA WA BAISKELI MAALUM KWA MWANAFUNZI WA SEKONDARI RUANDA

Damian Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Ruanda mara baada ya kukabidhiwa baiskeli maalum ya kutembelea.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimetoa msaada wa baiskeli maalum ya kutembelea mlemavu Damian Kapinga (22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya sekondari Ruanda wilayani humo yenye thamani ya shilingi milioni moja.

Akikabidhi msaada huo shuleni hapo mbele ya Mkuu wa shule Stephano Ndomba na Diwani wa viti maalum tarafa ya Namswea Immaculatha Mapunda, Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa Martin Mbawala alisema kuwa baiskeli hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na chama, kutoka kwa wasamaria wema.

Mbawala alisema kuwa chama kimefanya jitihada ya kutafuta baiskeli hiyo kutokana na taabu alizokuwa akizipata mtoto huyo kutambaa kwa mikono na magoti wakati wa kwenda shule kuhudhuria masomo yake, hivyo kiliona kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kumrahisishia asiendelee kupata adha hiyo.

“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia uweze kutembea na kuhudhuria masomo yako vizuri, nawaomba viongozi wa kata hii ya Ruanda muendelee kumtunza mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana matatizo ya ulemavu”, alisisitiza Mbawala.


Kwa upande wake mwanafunzi Damian alitoa shukrani kwa CHAWATA tawi la Mbinga, kumpatia msaada huo ambapo alisema ni mkombozi mkubwa kwake kwani awali alikuwa akipata shida namna ya kutembea hasa nyakati za masika pale mvua zinaponyesha.

Damian alieleza kuwa wakati huo wa mvua hasa pale zinaponyesha, wanafunzi wenzake walikuwa wakilazimika kumbeba na kumpeleka darasani ili aweze kuhudhuria masomo yake.


Vilevile Diwani wa viti maalum, Mapunda akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake waliokuwa wamewasili wakati wa kupokea kiti hicho cha kutembelea mwanafunzi huyo alitoa shukrani kwa Chama hicho cha walemavu tawi la Mbinga kuona umuhimu wa kumsaidia mtoto huyo, huku akiongeza kuwa msaada kama huo uendelee kutolewa kwa walemavu wengine pale panapojitokeza fursa ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kusaidia watu wenye ulemavu.

No comments: