Tuesday, November 15, 2016

WALIOKAMATWA WAKITOROSHA KAHAWA MBINGA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kassian Nyandindi,                   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba katika tuhuma ambazo zimefikishwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, juu ya suala la utoroshaji wa zao la kahawa ni lazima shauri hilo lifikishwe Mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

Cosmas Nshenye.
Aidha alisema kuwa ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya Watendaji wa serikali kushindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo juu ya namna ya kudhibiti hali hiyo, hatua ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine wafanyabiashara wajanja kutumia mwanya huo kuvunja sheria zilizowekwa na serikali wakiwa na lengo la kukwepa kulipa kodi au ushuru halali kwa mujibu wa sheria.

Nshenye alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia kukamatwa kwa mfanyabiashara, Khatwib Rajabu mkazi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera akidaiwa kushirikiana na wenzake kufanya tukio la utoroshwaji wa kahawa wilayani hapa, bila kufuata taratibu na sheria husika zilizowekwa na serikali.

“Hapa kesi lazima iwepo na kama sio kwa mfanyabiashara aliyehusika kutorosha kahawa basi itabaki kwa watumishi wa serikali waliohusika kutoa kibali hiki, huku wakijiua kwamba wanafanya makosa”, alisisitiza Nshenye.


Kwa ujumla taarifa za uhakika zilizomfikia mwandishi wetu kupitia vyanzo mbalimbali vya habari zinathibitisha kuwa gari lenye namba za usajili T 533 BLR na T 188 BGH mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini, Godfrey Malila ndilo lililohusika kwa namna moja au nyingine katika kutorosha kahawa hiyo yenye kudaiwa kuwa ni zaidi ya tani 50.

Wataalamu kutoka idara ya kilimo halmashauri ya mji wa Mbinga, ndio wanaonyoshewa kidole wakituhumiwa kuhusika juu ya utoroshaji huo ambapo mnamo Novemba 9 mwaka huu majira ya mchana, waliokuwa wakitorosha kahawa hiyo walikamatwa katika geti la mazao lililopo kijiji cha Kitai kata ya Mkako wilayani Mbinga.

Awali Mkuu wa wilaya hiyo, Nshenye katika vikao vyake mbalimbali vya kikazi amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kwamba, mtumishi yeyote ndani ya wilaya hiyo asiyetaka kubadilika kwa kuongeza uwajibikaji mzuri mahali pake pa kazi ni vyema akatafuta kazi nyingine ya kufanya au kwenda wilaya nyingine, lakini sio kubaki Mbinga ambayo imekuwa na historia nzuri ya wananchi wake kupenda kujituma kufanya kazi za kujiletea maendeleo bila kusukumwa.

Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akisema hayo kwa kupiga marufuku juu ya utoroshwaji wa zao la kahawa ambao umekuwa ukifanywa mara kwa mara kwa njia za ujanja wilayani humo na kuifanya wilaya hiyo kukosa mapato yake.


Hata hivyo jeshi la Polisi mkoani hapa, limethibitisha kukamatwa kwa shehena hiyo ya kahawa na gari lililobeba zao hilo ambapo imeelezwa kuwa watuhumiwa waliohusika kufanya hivyo wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani, ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili mbele yao.

No comments: