Tuesday, November 1, 2016

MADIWANI MBINGA WALALAMIKIA TATIZO LA UPUNGUFU WA MADAWA KATIKA VITUO VYA AFYA



Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikia kuwepo kwa tatizo kubwa la upungufu wa madawa na vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo wilayani humo, jambo ambalo linawafanya wagonjwa wengi washindwe kupatiwa matibabu.

Baadhi yao walisema kuwa licha ya kusikia matangazo kupitia vyombo vya habari kutoka kwa Waziri mwenye dhamana kwamba hakuna tatizo la upungufu wa madawa katika hospitali na vituo hivyo vya afya hapa nchini, hali hiyo imekuwa kinyume ndani ya wilaya hiyo ambapo maeneo mengi wagonjwa wanashindwa kupatiwa matibabu kutokana na kukosekana kwa madawa hayo.

Walifafanua kuwa hata kwa upande wa wanachama wa Mfuko wa bima ya afya (CHF) wengi wao hawapatiwi matibabu ipasavyo kutokana na sehemu ambako wanatolea huduma za afya kutokuwepo kwa madawa na vifaa tiba, jambo ambalo Madiwani katika kata zao wanashindwa kuendelea kuhamasisha wananchi wao waendelee kuchangia mfuko huo.


Hayo yalisemwa na Madiwani hao katika kikao chao cha baraza kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa na kuongeza kuwa, tatizo hilo sasa limekuwa sugu hivyo kuna kila sababu ya kulitafutia ufumbuzi wa haraka ili kuweza kumaliza kero hiyo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti sisi katika maeneo yetu hivi sasa tunashindwa hata kuhamasisha hawa wananchi kuendelea kuchangia katika mfuko huu wa bima ya afya, tunapokuwa kwenye mikutano pale tunapozungumzia suala hili tunazomewa na kuambiwa kwamba hata pale wanapochangia fedha zao hawapatiwi matibabu, hivyo tunaitaka serikali ione namna ya kuweka sawa jambo hili”, alisema Kelvin Kapinga diwani kata ya Nyoni.

Kwa upande wake akijibu hoja hiyo iliyotolewa na madiwani hao Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa alieleza kuwa tayari kuna baadhi ya dawa zimeletwa na bohari kuu ya madawa ambapo zitaanza kusambazwa hivi karibuni ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

No comments: