Tuesday, November 8, 2016

DC TUNDURU AWATAKA WANANCHI KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KWA KUJITUMA KUFANYA KAZI

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akisisitiza jambo katika mikutano yake ya hadhara wilayani hapa hivi karibuni.
Na Muhidin Amri,              
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera amewataka wananchi wa wilaya hiyo kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwa kujikita zaidi katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao badala ya kutumia muda wao mwingi, kupiga porojo za kisiasa ambazo zimeshapita muda wake.

Aidha Homera, amewahimiza kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wakati serikali nayo ikijiandaa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, jambo ambalo litasaidia kuongeza uzalishaji mashambani.

Ametaoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika ziara yake ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji mbalimbali vya kata ya Malumba, Nakapanya, Nandembo na Mpanji wakati akikagua pia zoezi la ufyatuaji tofari kwa kila kijiji wilayani humo.


Pia Mkuu huyo wa wilaya, alitembelea shule ya sekondari Nandembo ambapo aliwakumbusha wanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo kusoma kwa bidii na kuwa wazalendo katika nchi yao, kama alivyosisitiza Baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake.

Mbali na hilo, alikutana pia na vikundi vya wanawake na vijana waliojiunga kwenye vikundi vya Vicoba na kuwataka makundi mengine ya kijamii hususani wakulima nao kuunda vyama vya akiba na mikopo, ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Kutokana na hilo Mkuu wa wilaya, Homera alisema kuwa wananchi hao watakaojiunga katika vikundi hivyo serikali ipo tayari kuwaunga mkono kwa namna moja au nyingine ili waweze kusonga mbele kimaendeleo na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

No comments: