Saturday, November 5, 2016

MCHOMORO NAMTUMBO WAPEWA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI ZAHANATI

Na Mwandishi wetu,           
Namtumbo.

WANANCHI wa kijiji cha Mchomoro wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wamepata msaada wa vifaa vya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho kutoka kwa Kampuni inayotarajia kuchimba madini aina ya Uranium, Mantra Tanzania wilayani humo vyenye thamani ya shilingi milioni 16,329,000. 

Vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo ilikabidhi ikiwa ni mchango wake katika kuungana na wananchi wa kijiji hicho, kwa lengo la kukamilisha ujenzi wake ili uweze kukamilika kwa wakati husika uliopangwa.

Ofisa habari wa Kampuni hiyo, Khadija Pallangyo ndiye aliyekabidhi vifaa vya ujenzi kwa uongozi wa kijiji cha Mchomoro ambapo alitoa msaada wa bati 425, saruji mifuko 400, nondo 51, misumari na waya kilo 40, boriti 10 na mbao 20.


Pallangyo kwa upande wake aliutaka uongozi wa kijiji hicho kutumia vizuri vifaa hivyo kwa lengo lililokusudiwa na sio kuingiza ubinafsi wa kutaka kujinufaisha watu wachache.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Namtumbo, Laberto Mbilinyi pamoja na mambo mengine aliutaka uongozi wa kijiji hicho kusimamia kwa umakini mkubwa juu ya matumizi ya vifaa hivyo, ili kuwafanya hata wale wanaotoa misaada waweze kuwa na moyo endelevu katika kusaidia wananchi.

Kwa ujumla kijiji cha Mchomoro kimeomba kujenga kituo cha afya ambapo kwa hatua ya awali kinatarajia kuanza na ujenzi wa zahanati kutokana na kijiji hicho kukosa huduma za afya kwa wananchi wake kwa muda mrefu sasa.


Hata hivyo Mchomoro kuna jumla ya kaya 897 na wakazi 8,531 ikiwa wanaume ni 4,122 na wanawake 4,409 huku kikiwa na jumla ya vitongoji saba.

No comments: