Sunday, November 27, 2016

MBUNGE WA TUNDURU KUSINI AMWAGA NEEMA KWA WANANCHI WAKE


Na Julius Konala,     
Tunduru.

MBUNGE wa Jimbo la Tunduru kusini mkoani Ruvuma, Daimu Mpakate ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100 ili viweze kutumiwa na wananchi wake jimboni humo, kwa ajili ya kuwaletea maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Daimu Mpakate.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo alisema kuwa miongoni mwa misaada iliyotolewa ni mashine nane za kusaga nafaka zenye thamani ya shilingi milioni 16, vitabu vya kiada na ziada kwa shule za sekondari vyenye thamani ya shilingi milioni 32, mashine za kushonea nguo (vyerehani) nane vyenye thamani ya shilingi milioni 2, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 2 kwa ajili ya kugharimia kushona sare za shule kwa wanafunzi 120 watakaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.

Mpakate alitoa msaada huo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya serikali ya kijiji cha Mbesa wilayani humo ambapo vifaa hivyo vilitolewa kwa matumizi ya jamii kupitia shule nane za sekondari ambazo ni Nalasi, Mbesa, Mchoteka, Malumba, Ligoma, Lukumbule, Namasakata na Semeni.


Vifaa vingine vilivyokabidhiwa katika mkutano huo ni pamoja na magodoro 30 yenye thamani ya shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kuwasaidia wauguzaji wa wagonjwa ambao hulazwa katika hospitali ya Misheni Mbesa ambao hapo awali walikuwa wakilala chini.
Mbunge huyo aliongeza kuwa katika bajeti yake, ametenga pia jumla ya shilingi milioni 80 ambazo zitatoka katika mshahara wake kwa lengo la kuwasaidia na kuwahudumia wananchi wa jimbo la Tunduru kusini.

Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera pamoja na kumpongeza kwa juhudi anazozifanya Mbunge huyo alisema kuwa wapo wabunge wengi ambao wanaouwezo wa kusaidia wananchi wao, lakini wamekuwa hawawezi kujitoa kwa moyo katika kuchangia shughuli za maendeleo kwenye majimbo yao.

“Wakati wa kampeni baadhi ya wabunge wamekuwa wakitoa ahadi nyingi kwa wananchi wao, lakini baada ya kushinda tu chaguzi zilizopita matokeo yake huwa ni kinyume kutokana na wengi wao kushindwa kutimiza ahadi walizotoa kwa wananchi wao”, alisema Homera.

No comments: