Friday, November 11, 2016

WAZIRI MKUU AONGOZA BUNGENI KUUAGA MWILI WA MAREHEMU SAMUEL SITTA

Na Waandishi wetu, 
Dodoma.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza mamia ya wabunge, viongozi wa kitaifa na watumishi wa Ofisi ya Bunge kuuaga mwili wa Spika Mstaafu, Samwel Sitta.

Sitta alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 7 mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo Bungeni mjini Dodoma leo Novemba 11 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, mke wa marehemu Sitta, Margareth Sitta, mama wa marehemu Hajat Zuena Fundikila na familia ya marehemu na wabunge wote.

“Nitumie fursa hii pia kukupa pole Mheshimiwa Spika kwa pigo ambalo Bunge lako tukufu imelipata kwa kumpoteza mmoja wa viongozi mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu,

“Msiba uliotupata wa Spika huyu mstaafu wa Bunge la tisa (2005-2010) na Mbunge mstaafu wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora ni mzito”, alisema Majaliwa.

Alisema kuwa Sitta alikuwa ni mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

“Serikali imepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa, historia ya mzee Sitta ni pana sana, tunatambua utumishi wake uliotukuka katika nyadhifa mbalimbali alizozitumikia tutamkumbuka kwa utumishi wake,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Watanzania tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu kila mtu kwa imani yake ili tuweze kufikia japo mema machache aliyoyatenda katika enzi za uhai wake.

Enzi za uhai wake, Marehemu Sitta alibahatika kufanya kazi na marais wa awamu ya nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa mbunge kwa miaka 30.

Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri anayesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (wapili kulia) akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sitta kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sitta kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na viongozi wengine wakiusubiri mwili wa Spika mstaafu, Samuel Sitta uteremshwe kwenye ndege katika uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016
Mwili wa Spika Mstaafu Samuel Sitta ukiteremshwa kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016.
Mwili wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta ukiingizwa bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016. 
Mwili wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta ukiingizwa bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Mwili wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta ukiingizwa bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao maalum cha bunge cha kumuenzi Spika Mstaafu, Samuel Sitta, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu Mstaafu, Samuel Malecela akimpa pole mjane wa Spika Mstaafu, Margareth Sitta bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye jeneza la Spika Mstaafu Samwel Sitta, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Spika Mstaafu, Samuel Sitta, bungeni mjini Dodoma, Novemba 11, 2016. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)​

No comments: