Tuesday, November 1, 2016

JESHI LA POLISI RUVUMA LINAWASAKA MAJAMBAZI WALIOPORA MILIONI 15 ZA MFANYABIASHARA KIGONSERA MBINGA



Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linawasaka watu watano wanaodaiwa kuwa ni majambazi ambao walivamia duka la Mfanyabiashara mmoja anayefahamika kwa jina la Msafiri Tullo (40) mkazi wa mji mdogo wa Kigonsera wilayani Mbinga mkoani humo na kumpora fedha taslimu za mauzo shillingi milioni 15,250,000 pamoja na simu mbili za kiganjani aina ya Tecno, zenye thamani ya shilingi 110,000 na kutokomea kusikojulikana.
Zubery Mwombeji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1:30 jioni katika mji huo wa kigonsera.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo palitokea kundi la watu watano huku wakiwa na silaha za jadi ambazo walikuwa wameshika mkononi, ambapo walipowasili dukani hapo walianza kumshambulia Msafiri kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kufanikiwa kumpora fedha hizo huku wakimjeruhi sikio lake la upande wa kushoto na muuzaji wake wa duka hilo, Melkion Nchimbi (18).


Alisema kuwa majambazi hao walikuwa na silaha za jadi virungu na mapanga ambapo baada ya kupora fedha hizo waliondoka huku wakikimbia na kuelekea kusikojulikana na kwamba Majeruhi hao, walikimbizwa katika kituo cha afya Kigonsera ambacho ni cha Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga ambako walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi makwao.

Kamanda Mwombeji alieleza kuwa Polisi mkoani Ruvuma, hivi sasa inawasaka watuhumiwa hao ambao wanadaiwa kukimbilia kwenda Songea mjini na pale watakapofanikiwa kuwakamata watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments: