Tuesday, November 8, 2016

WANANCHI RUANDA WAKUMBWA NA MAAFA YA KUEZULIWA NYUMBA ZAO RC RUVUMA ASIKITISHWA OFISI YAKE KUTOPEWA TAARIFA KWA WAKATI

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

JUMLA ya Kaya saba zenye wakazi zaidi ya 40 waishio katika kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamekosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo mkali.

Tukio hilo lilitokea Novemba Mosi mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika kata hiyo, huku wengine baadhi yao nyumba zao zikiwa zimenusurika kubomolewa baada ya kuezuliwa na upepo huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema kuwa jumla ya nyumba 32 za wananchi ziliezuliwa na upepo huo.


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge ambaye alitembelea katika eneo la tukio hilo Novemba 8 mwaka huu akiwa ameambatana na waandishi wa habari, alisikitishwa na uongozi wa wilaya hiyo kwa kuchelewesha kutoa taarifa ya tukio hilo ambapo alikemea hali hiyo na kutaka isijirudie tena.

Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Mahenge baada ya kupata taarifa za tukio hilo, kutoka kwa wasamaria wema ilichukua jukumu la kutembelea wananchi hao waliokumbwa na maafa hayo.

“Nimesikitishwa sana na kitendo cha viongozi wa wilaya hii kuchelewesha taarifa za tukio hili ofisini kwangu, hawa watu wamepatwa na maafa siku kadhaa zilizopita wanahitaji kupatiwa msaada”, alisema Dkt. Mahenge.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema kuwa katika nyumba hizo 32 za wananchi zilizoezuliwa, nyumba tatu ni za taasisi za umma ikiwemo ofisi ya Kata, Mahakama ya mwanzo na kwamba hadi sasa kaya saba hazina uwezo wa kuezeka tena nyumba zao huku tathimini ya awali ikionesha kwamba wamepata hasara ya milioni 14.

Nao kwa upande wao baadhi ya wananchi waliokumbwa na maafa hayo wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia haraka kwani hawana mahala hata pa kulala.


Hata hivyo baada ya kutembelea waathirika wa tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge pamoja na kuahidi kusaidia wananchi hao baada ya tathimini kukamilika, lakini pia amesisitiza ujengaji wa nyumba imara za kisasa ili waweze kuepukana na majanga kama hayo ambayo yanaweza kujitokeza tena hapo baadaye.

No comments: