Thursday, November 10, 2016

MWILI WA MAREHEMU SAMUEL SITTA WAWASILI JIJINI DAR


Na Mwandishi wetu;

MWILI wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta umewasili jioni hii leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, ukitokea nchini Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.

Mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege, mwili wa Marehemu Sitta umepelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.


Taarifa zilizotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Gerald Mongella, zinasema kwamba;

Kesho, Ijumaa saa tatu asubuhi kutakuwa na ibada ya kuuaga mwili huo katika Viwanja vya Karimjee ambako ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam watapata fursa ya kumuaga.

Baadaye mwili wa Marehemu Sitta, utasafirishwa kwenda mkoani Dodoma ambako utaagwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kisha kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora, kwa mazishi yatakayofanyika Jumamosi.

Marehemu Sitta alifariki dunia Novemba 07 mwaka huu katika Hospitali ya Technal University iliyopo nchini Ujerumani, alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya tezi dume.


MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI, AMEN.

No comments: