Thursday, November 10, 2016

NSHENYE AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI MBINGA WANAOSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO WAJIONDOE MAPEMA

Na Kassian Nyandindi,                   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya watendaji wa serikali wilayani humo wanaoshindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo hatua ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine, wananchi wazivunje kwa kukataa kutii maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa serikali.
Cosmas Nshenye.

Nshenye alitolea mfano kwa agizo la serikali kuzuia uuzaji na unywaji wa pombe saa za kazi, hata hivyo mamlaka zinazohusika kusimamia hilo kama vile jeshi la Polisi na halmashauri kupitia kitengo chake cha biashara wahusika wamekuwa wakikaa kimya bila kuchukua hatua.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza maafisa biashara wa halmashauri ya wilaya na mji wa Mbinga, kuwakamata na kuwapiga faini au kuwafutia leseni wale wote wanaofanyabiashara ya kuuza pombe saa za kazi.

Alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Nshenye aliwataka pia watumishi wa umma kutimiza wajibu wao ipasavyo pasipo kusubiri kusukumwa  kwani  ni kosa kwa mtumishi wa serikali kushindwa kuleta tija eneo lake la kazi kwani serikali ya awamu ya tano, tangu ilipoingia madarakani imedhamiria kuleta mabadiliko makubwa kwa Watanzania ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na maisha bora kwa wananchi wake kwa kuwapatia huduma zilizokuwa bora.


Alisema kuwa kwa mtumishi asiyetaka kubadilika kwa kuongeza uwajibikaji mzuri mahali pake pa kazi ni vyema akatafuta kazi nyingine ya kufanya au kwenda wilaya nyingine, lakini sio kubaki Mbinga ambayo imekuwa na historia nzuri ya wananchi wake kupenda kujituma kufanya kazi za kujiletea maendeleo bila kusukumwa.

Katika hatua nyingine Nshenye amepiga marufuku kwa vijana wanaoosha magari kufanya shughuli hizo katika mito ambayo inatiririsha maji kwenda katika maeneo mbalimbali waondoke katika maeneo hayo haraka kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kutunza afya za binadamu kwani itazuia hatari ya binadamu kupata magonjwa mbalimbali ambayo yanatokana na kunywa maji machafu ambayo huchafuliwa kwa takataka wakati wa kuosha magari kwenye vyanzo hivyo.

“Kazi hizi za kuosha magari zifanywe katika maeneo maalumu yaliyotengwa na kujengwa ‘Car wash’ ili hata halmashauri iweze kukusanya mapato yake, badala ya kufanywa katika maeneo ambayo sio rasmi”, alisisitiza Nshenye.


Vilevile amemtaka Ofisa mazingira wa halmashauri ya mji wa Mbinga kusimamia jambo hilo kwa kuhakikisha wale wote waliopo katika maeneo ya vyanzo vya maji wanaondolewa haraka kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

No comments: