Sunday, November 6, 2016

DC MBINGA APIGA MARUFUKU UNYWAJI POMBE SAA ZA KAZI AMTAKA AFISA BIASHARA KUNYANG'ANYA LESENI KWA WANAOKAIDI

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amepiga marufuku unywaji pombe saa za kazi na kumtaka Afisa biashara mwenye dhamana ya kusimamia suala hilo, ahakikishe kwamba anadhibiti hali hiyo ili isiweze kuendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Nshenye alitoa rai hiyo juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo aliagiza pia kuwashughulikia wale wote ambao wanauza pombe saa za kazi asubuhi.

“Leseni za biashara naagiza zinyang’anywe kwa wale wanaouza pombe saa za asubuhi, haiwezekani watu wanaacha kufanya kazi badala yake utaona wanakwenda kwenye baa na kunywa pombe, pombe zote zianze kunyweka kuanzia saa tisa jioni”, alisisitiza Nshenye.

Aliongeza kuwa kwa wale watumishi ambao watashindwa kusimamia majukumu ya kazi zao ipasavyo, wajiandae kuacha kazi au wajiondoe mapema wenyewe kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.


Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa muda wa mtumishi kufanya kazi kwa mazoea umepita, hivyo ni wakati wa kutimiza majukumu ya kazi zao ili jamii iweze kunufaika na huduma zinazotolewa na serikali.

Kadhalika kupitia baraza hilo la Madiwani, Nshenye alitoa agizo kwa kuwataka pia wananchi wale wote wanaosha magari kwenye vyanzo vya maji waondoke mara moja katika maeneo hayo kwani huo ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira.

“Ninatoa agizo kwa Afisa mazingira asimamie hili kwa sababu ndio wajibu wake, kamata gari lolote lile linalooshwa mtoni lipelekwe ofisi za halmashauri lipigwe faini, tusigombane na waosha magari tugombane na wamiliki wa magari”, alisema.


Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Ndunguru Kipwele kwa upande wake alimhakikishia Mkuu huyo wa wilaya kwamba maagizo hayo aliyoyatoa atahakikisha anayasimamia ipasavyo na kufanyiwa utekelezaji ili yaweze kuzaa matunda.

No comments: