Sunday, November 16, 2014

CHEMBA YA WAFANYABIASHARA MBINGA YAITAKA SERIKALI ULIPAJI KODI UFANYIKE MAHALI BIDHAA INAPOZALISHWA, GAUDENCE KAYOMBO LAWAMANI


Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

UMOJA wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, umepanga mikakati na kuitaka serikali iweke taratibu zake ambazo zitahakikisha kwamba, kila jambo la ulipaji wa kodi lifanyike pale mahali ambapo bidhaa inazalishwa kwa lengo la kukuza uchumi wa eneo husika na Taifa kwa ujumla. 

Aidha kodi za makampuni yanayofanya kazi au biashara yoyote wilayani humo, malipo yafanyike Mbinga ikiwa ni lengo la kumfanya mfanyabiashara mkubwa na mdogo, asiweze kuumizwa kwa kutozwa kodi kubwa.

Hayo yalisemwa katika kikao cha Wafanyabiashara hao kilichoketi ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mjini hapa, ambapo walieleza kwamba wafanyabiashara wa wilaya hiyo hutozwa kodi kubwa ya mapato kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, ambapo walitolea mfano kwa wale ambao hujishughulisha na ununuzi wa zao la kahawa wilayani humo, kwenda makao makuu ya kampuni zao yaliyopo nje ya Mbinga kulipia kodi zao. 

Vilevile mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Menlick Sanga, aliongeza kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na mwekezaji mkubwa wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka, ambayo uchimbaji wake hufanyika katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Rwanda wilayani humo, bado amekuwa halipi kodi hapa wilayani na wilaya kutonufaika na chochote hivyo ni vyema serikali ikaliangalia hilo ili malipo husika kwa mwekezaji huyo aweze kuyafanya hapa hapa wilayani.


“Sawa tunajua sheria inasema ulipaji wa kodi kwa kampuni yoyote inaruhusiwa kulipa makao makuu ya kampuni husika, lakini sisi kama jumuiya ya wafanyabiashara hapa Mbinga, tunatakiwa tusimame kidete kwa kuiomba serikali itusaidie katika hili”, alisema.

Walisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa utoroshaji wa mapato ya wilaya, hivyo serikali ni vyema ikaridhia ulipaji wa kodi zao ukafanywa hapa Mbinga kwa lengo la kuongeza hata mapato ya ndani na taifa kwa ujumla ili baadaye wafanyabiashara hao waweze kuondokana na adha wanayoipata sasa ya kutozwa kodi kubwa ya mapato.

Katika hatua nyingine walimtaka Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kufanya kikao na wafanyabiashara wa wilaya hiyo, ili aweze kukusanya maoni na kero zao.

Mjumbe mmoja katika kikao hicho aliyejitambulisha kwa jina la Dominic Migambo alimlalamikia Mbunge huyo akisema, inamshangaza kuona tokea Kayombo achaguliwe na kuingia madarakani kuliongoza Jimbo hilo, hajawahi kufanya kikao na wafanyabiashara wa wilaya ya Mbinga jambo ambalo alihoji kero au matatizo yao atawezaje kuyafahamu na kuyafikisha Bungeni, ili yaweze kufanyiwa kazi.

“Huyu Kayombo tokea aingie madarakani sisi wafanyabiashara amekuwa hatujali hata siku moja, hajawahi kutuita pamoja na  kufanya naye kikao ili aweze kujua matatizo yetu”, alisema Migambo.

Pamoja na mambo mengine wafanyabiashara hao wilayani humo, waliweza pia kupanga taratibu za kukuza ofisi ya umoja wao kwa kuhakikisha kila mmoja wao anajitoa kwa moyo, katika kuchangia ada na michango mbalimbali pale inapohitajika ili waweze kusonga mbele kwa faida ya sasa na baadaye.

No comments: