Monday, June 29, 2015

UVCCM NYASA YAWATAKA WANACHAMA WAKE KUJENGA USHIRIKIANO


Wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamekusanyika pamoja kumsikiliza Kamanda wao wa Umoja huo, Cassian Njowoka.

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Cassian Njowoka akiwa na wanachama wake wa umoja huo ambapo mbele yao kuna moja kati ya kikombe ambacho hukitoa zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mpira wa miguu katika timu mbalimbali, ambazo huendelea kushindana wilayani humo. Hapo tukio hilo lilifanyika jana katika kata ya Liuli wilayani Nyasa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

ZIARA ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, imeendelea kung’ara na kushika kasi katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kufuatia wanachama wa umoja huo kujitokeza kwa wingi katika kila eneo la mapokezi yanapofanyika.

Njowoka ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani humo, ikilenga kutembelea timu za mpira wa miguu na ambazo zinashiriki ligi kuu ya UVCCM wilayani humo, maarufu kwa jina la Njowoka Cup pamoja na kuongea na wanachama wa umoja huo.

Washiriki wa ligi hiyo amekuwa akiwapatia zawadi ya vifaa vya michezo kama vile kikombe kimoja cha ushindi, jezi seti tatu na mpira mmoja kwa mshindi wa kwanza, jezi seti mbili na mpira mmoja kwa mshindi wa pili na seti moja ya jezi kwa mshindi wa tatu.
Haya yote yanajiri kufuatia ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni katika zoezi lake la kuwasimika makamanda wa UVCCM kwa kila kata za wilaya hiyo.


Aidha licha ya kufanya hivyo, pia amekuwa akichangia vifaa katika vituo vya afya na zahanati zilizopo wilayani humo ambapo vitanda, mashuka ya kulalia, vyandarua kwa pamoja vimekuwa vikitolewa kwenye maeneo hayo ili viweze kusaidia wananchi.

Wilaya ya Nyasa ambayo hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa katika huduma ya afya, Kamanda huyo wa UVCCM ameapa kuendelea kusaidia katika sekta hiyo muhimu ili jamii iweze kuondokana na kero hiyo kwa kuchangia shughuli za ujenzi na vifaa muhimu vya matibabu.

"Nitaendelea kusaidia ndugu zangu wa huku Nyasa, sisi sote tunapaswa kuungana ili tuweze kufikia malengo, wilaya yetu inachangamoto nyingi ambazo zinahitaji kuungana pamoja ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea", alisema Njowoka.


Hata hivyo ziara hiyo ambayo ilianza mapema Juni 25 mwaka huu katika kijiji cha Ngindo kata ya Lipingo, anatarajia kuhitimisha mzunguko wake kwa wilaya yote ya Nyasa ifikapo Julai 14 mwaka huu katika kijiji cha Ndondo kata ya Liparamba wilayani humo.

No comments: