Sunday, May 31, 2015

MANISPAA SONGEA NA MIKAKATI YA KUBORESHA MATIBABU KWA WAZEE

Na Muhidin Amri,
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imekuwa ikitenga kiasi cha shilingi milioni 10 kila mwaka, ikiwa ni lengo la kuhakikisha kwamba wazee wanaoishi katika Manispaa hiyo wanapatiwa matibabu ipasavyo, wakiwemo na wategemezi wao.

Fedha hizo zinazotengwa hugharimia matibabu ya wazee 600 na wategemezi wao 2700, ambao hunufaika na mpango wa matibabu bima ya afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali zilizopo katika Manispaa hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii mkoani Ruvuma (CHF) wa Manispaa ya Songea, Victor Nyenza alipokuwa akizungumza kwenye mdahalo wa wazi uliohusu usalama wa wazee hapa nchini, ambao ulifanyika mjini hapa.


Mdahalo huo ulikuwa umeandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la PAD Nyanda za juu kusini, ambapo Nyenza alifafanua kuwa vituo vya kutolea huduma ya afya 16 vilivyopo katika Manispaa hiyo ndivyo ambavyo vimetengwa kwa ajili ya kutolea huduma ya matibabu kwa wazee hao.

Alisema kuwa wametengewa vyumba maalum kwa ajili ya kupatiwa huduma husika na wagaganga wakuwahudumia, pale wanapohitaji kupatiwa tiba.

Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, imeanzisha mpango wa kugharimia matibabu hayo kwa wategemezi ambao huwatunza wazee hao, hasa kwa wale waliokuwa chini ya umri wa maika 18 na yatima.

Nyenza alieleza kuwa hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu, tayari jumla ya kaya 1,419 za wazee wenye wategemezi 6,795 zinahudumiwa na wamepatiwa vitambulisho vya CHF.

Alibainisha kuwa kaya 819 hupata matibabu katika vituo vya serikali, na wazee wengine waliobakia hupatiwa huduma hiyo kwenye zahanati za watu binafsi na mashirika ya dini.


Katika kuimarisha huduma hiyo, Manispaa ya Songea imekuwa ikiajiri watumishi wa kutosha wa idara ya afya ili kuweza kukabiliana na upungufu uliopo na tayari jumla ya watumishi wapya 42 wameajiriwa, kati ya hao 34 wameripoti katika vituo vyao vya kazi.

No comments: