Friday, May 1, 2015

WANANCHI TUNDURU WATESEKA NA MALARIA

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Njenga katika maadhimisho ya siku ya Malaria Africa.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEELEZWA kuwa asilimia 38.3 ya vifo vilivyotokea mwaka 2014 wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, vilitokana na ugonjwa hatari wa Malaria.

Hayo na mengine mengi, yalibainishwa katika taarifa iliyosomwa na mratibu msaidizi wa ugonjwa huo wilayani humo, Ayub Joseph katika maadhimisho ya siku ya Malaria Africa yaliyofanyika kijiji cha Njenga wilayani humo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa siku hiyo, jumla ya watu 487 waliripotiwa kupoteza maisha katika vituo vya kutolea huduma za afya wilayani Tunduru.

Akizungumzia mkakati wa kupambana na ugonjwa huo, Joseph alisema pamoja na uwepo wa juhudi hizo za kupambana na Malaria idara yake imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa madawa na vifaa tiba, ambavyo mgawo wake umekuwa ukitolewa bila kuzingatia uwiano na bohari ya dawa hapa nchini (MSD).


Joseph alifafanua kuwa katika kipindi hicho, pia vituo vyake vya afya wilayani humo, vilitoa huduma kwa wagonjwa wa nje 10,791 ambao waligundulika kuugua Malaria.

Takwimu ziliendelea kufafanua kuwa, kati ya wagonjwa 10,503 walipokelewa na kulazwa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali ambazo zipo katika wilaya hiyo, kati ya hao wagonjwa 5,893 walibainika kuwa na ugonjwa huo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Nalicho aliwataka wananchi mara kwa mara kutunza mazingira yao katika hali ya usafi ili waweze kuondokana na mazalia ya mbu, ambao hueneza ugonjwa huo.


Sambamba na kuyatekeleza hayo, aliwasihi waachane na mila potofu kwenda kwa waganga wa kienyeji hasa pale wanapojisikia wana homa kali, badala yake waende hospitali au katika vituo vya afya ambavyo vimewekwa na serikali, kwa ajili ya kuhudumia wananchi wake.

No comments: