Friday, May 29, 2015

WAHITIMU CHUO CHA SAYANSI WATAKIWA KUWAKOMBOA WATANZANIA

 
Upande wa kulia, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki la Songea mkoani Ruvuma, Damian Dallu akimzawadia kompyuta mpakato (Laptop) mmoja wa wahitimu wa chuo cha sayansi na tekinolojia ya mawasiliuano cha Mtakatifu Joseph mjini Songea ambaye amevaa vazi jeusi, baada ya kufanya vizuri masomo yake na kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Dokta Arulaj. 

Na Julius Konala,
Songea.

WAHITIMU wa chuo cha Sayansi na tekinolojia ya mawasiliano cha Mtakatifu Joseph, kilichopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa huko waendako kutumia vyema elimu waliyoipata, kwa malengo ya kuwakomboa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Aidha wameshauriwa kutumia kipawa walichonacho, kuongeza juhudi na maarifa waliyoyapata chuoni hapo ili waweze kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Rai hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea, Damian Dallu alipokuwa akizungumza na wanafunzi, wazazi na walimu kwenye mahafali ya sita ya chuo hicho yaliyofanyika mjini hapa.


Wahitimu zaidi ya 100 walitunukiwa vyeti vya stashahada na shahada na kwamba alipongeza uongozi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania, kwa kutoa mchango wake mkubwa kwenye nyanja ya elimu hapa nchini huku akiwataka wananchi kutumia chuo hicho kupata elimu bora zaidi, ambayo itasaidia taifa kupata wanasayansi wengi zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Tanzania, Padri Arulraj ameipongeza serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Kikwete na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu, kwa kutoa michango yao ambayo imesaidia kukua kwa chuo hicho.

Vilevile Rais wa chuo cha Mtakatifu Joseph Afrika, Dokta Ananth alisema mbegu njema iliyopandwa katika ardhi ya Tanzania mnamo mwaka 2003 imeweza kuzaa matunda mazuri kutokana na kufanikiwa kupata chuo kikuu, na kuongezeka kwa vyuo vitano vyenye jumla ya wanafunzi 8,000 hapa nchini.

Dokta Ananth alisema kuwa katika kipindi hiki cha mwaka 2015 wanatarajia kuanzisha vyuo vingine viwili, katika maeneo ya Sumbawanga na Boko Jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, wahitimu waliokuwepo kwenye mahafali hayo walielezea furaha yao wakisema watahakikisha elimu waliyoipata wanalisaidia taifa hili, hasa katika kipindi hiki cha ulimwengu wa sayansi na tekinolojia huku wakiiomba serikali kuwatumia pale zinapotokea fursa mbalimbali, hususani katika uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura (BVR).

No comments: