Monday, May 11, 2015

NJOWOKA ASAMBAZA VIFAA VYA MICHEZO NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANANCHI wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambao baadhi yao hujishughulisha na michezo ya mpira wa miguu na pete wameanza kunufaika kwa kupewa mipira, jezi na vifaa maalum vya michezo hiyo ili viweze kuwarahisishia wakati wanaposakata kandanda wilayani humo.

Vifaa hivyo vimetolewa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa, Cassian Njowoka alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wakati akitembelea kata mbalimbali za wilaya hiyo.

Njowoka ambaye hivi sasa ni ziara yake ya pili tangu aliposimikwa kuwa kiongozi wa UVCCM wa Nyasa na kwamba lengo kuu la ziara hiyo, pia ni kufungua ligi za michezo hiyo na kujionea changamoto mbalimbali ndani ya wilaya, hatimaye zipatiwe ufumbuzi.


 “Ndugu zangu michezo ni tunu ya taifa letu, tupende michezo kwa sababu imekuwa ikiimarisha hata viungo vyetu vya mwili na kutufanya tuishi vizuri bila kikwazo chochote”, alisema Njowoka.

Pamoja na mambo mengine, Njowoka alisema kuwa katika ukamanda wake wa jumuiya hiyo yupo tayari kuendeleza vipaji vya mchezo mpira wa miguu na pete wilayani Nyasa, ili kizazi hiki cha sasa na kijacho kiweze kunufaika. 


Jumla ya kata sita zimekabidhiwa vifaa hivyo vya michezo wilayani humo ambazo ni Mtipwili, Kilosa, Mbamba bay, Liuli, Lipingo,  na Kihagara kwa ajili ya kuanza kucheza ligi za mashindano ya mchezo mpira wa miguu na pete.

No comments: