Wednesday, May 27, 2015

WANACCM MBINGA KUMCHANGIA FOMU KELVIN MAPUNDA

Diwani wa kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, Kelvin Mapunda (Aliyevaa koti nyeusi) akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mbambi, Mbinga na Nyerere zilizopo katika kata hiyo wakati akiwa katika ziara yake hivi karibuni, akitembelea vituo vya masomo wakati wa likizo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BAADHI ya wazee na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wamemtaka Diwani wa kata hiyo Kelvin Mapunda kwenda kuchukua fomu muda utakapofika kwa ajili ya kugombea tena, nafasi ya udiwani katika kata hiyo.

Aidha walieleza kuwa wapo tayari kutoa fedha zao mfukoni kwa ajili ya kumchangia fomu ya kuwania nafasi hiyo, kwa kile walichoeleza kuwa wamejenga imani naye kutokana na kazi zake alizozifanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake aliowaongoza.

Wazee na vijana hao walisema hayo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini hapa, huku wakiongeza kuwa wao wanaona ndiye mwanachama ambaye yupo karibu nao katika kuendeleza maendeleo yao kwa faida ya sasa, na kizazi kijacho.


“Tokea aingie madarakani mwaka 2005 hadi sasa, tunaona ndiye kiongozi ambaye anapaswa kuendelea kutuongoza katika kata hii amekuwa akishirikiana na wananchi kwa mambo mbalimbali ya kijamii, hivyo hatuna budi kumpatia nafasi aendelee kutuongoza”, walisema.  

Waliendelea kueleza kuwa ushirikiano aliokuwa nao, wamependezwa hasa katika kupigania ujenzi wa barabara za lami na kituo cha kisasa magari ya abiria Mbinga mjini, kuboresha elimu, afya na mambo mengine ya kimaendeleo jambo ambalo linamfanya ang’are kuliko wengine.

Mapunda alipoulizwa na mtandao huu kama yupo tayari kugombea tena katika nafasi hiyo, alithibitisha kupokea maombi ya wazee na vijana wa CCM, huku akifafanua kwamba atatekeleza hilo pale muda utakapowadia.

“Ndugu yangu kwa sasa siwezi kuzungumza sana juu ya hili, lakini tuombe Mungu pale muda utakapowadia naweza nikazungumzia suala la kuendelea kuwaongoza wananchi wangu katika kata hii ya Mbinga mjini au la, wengi wamenifuata na kunitaka niendelee”, alisema Mapunda.


Pamoja na mambo mengine, serikali hapa nchini katika mpango wake wa kusogeza huduma karibu na wananchi, imeweza pia kuongeza kata katika mji wa Mbinga na kufikia kata nane ambazo ni Mbinga mjini A na B, Matarawe, Mbambi, Luhuwiko, Betlehemu, Masumuni na Lusonga ambazo kufikia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, watachaguliwa madiwani watakaoweza kuongoza kata hizo.

No comments: