Monday, May 18, 2015

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA FEDHA AWASHUKIA WATUMISHI WA UMMA


Waandishi na wadau mbalimbali wa habari kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, leo wakiwa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam, katika semina na maadhimisho ya miaka kumi ya Mamlaka ya udhibiti na manunuzi (PPRA)
Na Kassian Nyandindi,
Dar es Salaam.

IMEELEZWA kuwa watumishi wa umma kwa kushirikiana na watu binafsi hapa nchini, baadhi yao wamekuwa hawafuati  taratibu ambazo zinaongoza manunuzi katika sekta ya umma, kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha kuathiri ustawi wa maendeleo ya wananchi.

Aidha imeshauriwa kuwa uadilifu na uwazi katika kusimamia mfumo wa manunuzi ya umma ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa wakati wote, ili kuwezesha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha na matokeo yenye tija kijamii na kiuchumi.

Hayo yalisemwa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya fedha, Dorothy Mwanyika ambaye alikuwa akimwakilisha Naibu Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba katika semina ya siku moja iliyowakutanisha Waandishi na wadau wa habari.  

Semina hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi Tanzania (PPRA) ambayo pia inaadhimisha miaka kumi tokea ianzishwe hapa nchini, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.


“Katika kuandika habari za manunuzi ya umma waandishi wa habari mnao mchango mkubwa sana, kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ubadhirifu katika sekta hii, nawasisitiza endeleeni na mchango wenu wa kuibua maovu yanayofanywa katika sekta hii, ili muweze kujenga uwazi na uwajibikaji”, alisema Mwanyika.

Kadhalika alipongeza jitihada zinazofanywa na waandishi wa habari hapa nchini, katika kuripoti habari za maendeleo ya wananchi hasa kwa upande wa manunuzi ambako kwa kiasi kikubwa baadhi ya watumishi, katika taasisi husika au kamati za Halmashauri za wilaya wamekuwa wakitekeleza miradi chini ya kiwango.

Naibu katibu mkuu huyo alifafanua kuwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu na malipo hewa yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali na kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wadau, hivyo kusababisha hata ustawi wa maendeleo katika taifa hili kurudi nyuma kutokana na watumishi wasio waaminifu kutekeleza majukumu yao, kwa kutozingatia taratibu za utumishi wa umma.

Awali kwa upande wake Afisa mtendaji mkuu wa PPRA, Dokta Laurent Shirima alieleza kuwa Mamlaka hiyo tokea ianze kufanya kazi zake hapa nchini, tayari imekwisha yafungia kampuni 26 na kuyakataza kutofanya kazi tena ya manunuzi ya umma kutokana na kukiuka sheria, kanuni na taratibu husika.

“Ndugu zangu manunuzi ya umma sio kichaka cha watu kujitafutia fedha isiyo halali, tunahitaji taratibu zifuatwe kumekuwa na tatizo la kukosa uadilifu katika manunuzi, wizi, kukosekana kwa uadilifu na vitendo vya rushwa katika shughuli nzima ya kufanya manunuzi, mamlaka tutaendelea kupambana na mambo maovu haya”, alisema.

Dokta shirima aliongeza kuwa uzingatiaji wa haki, ushindani, uwazi, kutokuwepo kwa ubaguzi na upatikanaji wa thamani wa manunuzi ya umma ndio mambo muhimu, ambayo yanapaswa kuzingatiwa wakati wote.


Hata hivyo alifafanua kwamba, PPRA itaendelea kuzingatia viwango na ufuatiliaji wa sheria husika, kwa taasisi za ununuzi ikiwemo kuratibu, kuanzisha na kusimamia mfumo wa manunuzi kwa kutumia tekinolojia ya TEHAMA.

No comments: