Monday, May 4, 2015

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUACHA KUNUNULIWA NA WANASIASA

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAANDISHI wa habari nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kununuliwa na wanasiasa kwa lengo la kuandika habari zao ambazo zimekuwa zikiegemea upande mmoja na kusahau matatizo ya wananchi, jambo ambalo limekuwa likisababisha jamii kukosa imani nao.

Aidha imeelezwa kuwa jamii inatambua wajibu na mchango wa wanahabari, hivyo  ni chombo muhimu kinachopaswa kupongezwa wakati wote kutokana na kuibua mambo kadha wa kadha ambayo yakikaliwa kimya, nchi yetu inaelekea kubaya.

Hayo yalisemwa na Wakili wa serikali mwandamizi mkoani Ruvuma kanda ya Songea, Renatus Mkude alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa huo kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Masista mjini hapa.


Mkude ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, alisema kuwa upashanaji habari ni jambo muhimu hivyo vyombo vya habari vimekuwa vikijenga ustawi mkubwa wa maendeleo katika jamii na kwamba, kukua kwa tekinolojia duniani kumesaidia pia wananchi kupata habari kwa wakati na ubora wa hali ya juu.

“Ndugu zangu utawala wa sheria sio nchi tu kufuata sheria, bali kuwepo kwa sheria zinazozingatia haki hivyo nawasihi hata ninyi katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku zingatieni taratibu na sheria za kazi zenu, kwa kuitendea haki jamii hii ambayo inawazunguka”, alisema Mkude.

Vilevile alieleza kuwa waandishi wa habari waepuke kuandika habari za uzushi, ili kuepukana na machafuko yanayoweza kutokea baadaye ambapo wazingatie maslahi ya nchi na watu wake, kwa kufanya kazi zao kwa weledi.

“Nawasihi endeleeni kuibua maovu ili tuweze kuleta maendeleo, andikeni habari sahihi tuweze kujenga uwazi na wajibikaji katika jamii pia jengeni utamaduni wa kushirikiana na serikali, kuiwezesha kutimiza malengo yake”, alisema.

Hata hivyo aliongeza kwa kuwataka wanahabari, kutumia kalamu zao kuelimisha jamii juu ya mambo mtambuka na namna ya kupambana nayo, kama vile vita dhidi ya rushwa na utunzaji wa mazingira.


No comments: