Monday, May 4, 2015

TUNDURU ATAKAYELETA VURUGU KATIKA ZOEZI LA UANDIKISHAJI KUKIONA CHA MOTO

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imeapa kutofumbia macho kitendo chochote kitakachojitokeza juu ya uvunjifu wa amani katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ambalo hivi sasa linaendelea wilayani humo.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapa, Chande Nalicho ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza hivi karibuni, katika maadhimisho ya sherehe za wafanyakazi zilizofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba, amechukua hatua ya kutoa tamko hilo kufuatia taarifa za kiintelejensia ambazo zimemfikia ofisini kwake kuwa, kuna mbinu chafu zinasukwa chini kwa chini na watu wenye nia mbaya kwa lengo la kutaka kuleta vurugu ili zoezi hilo lisiweze kufanikiwa kama ilivyopangwa.


“Kuna taarifa tumepata kuwa kuna kundi la vijana ambao wanafadhiliwa na vyama vya upinzani, wanataka kutuharibia zoezi hili kwa vurugu wanazotaka kuzianzisha ambazo hazina msingi wowote, sasa wakifanya hivyo hakika na waambieni serikali haitalifumbia macho jambo hili watakiona chamtemakuni”, alisema Nalicho.

Nalicho alifafanua kuwa vijana hao wanataka kuwazuia wazee katika vituo hivyo vya kujiandikisha ili wasijiandikishe, kwa madai kwamba wamekuwa wakiwachagua viongozi wa CCM katika chaguzi mbalimbali ambao hawawaletei maendeleo.

Awali akizungumzia juu ya maadhimisho ya sherehe za wafanyakazi, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka waajiri kuachana na tabia ya kuwatumikisha watumishi wao bila kuwapatia maslahi yao, badala yake watimize wajibu wa kutoa haki zinazostahili ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Naye Katibu wa Muungano wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) wilayani Tunduru, Kassim Dini aliwataka viongozi wilayani humo kubadilika katika utendaji wa kazi zao na kuiga mfano mzuri unaofanywa na viongozi wa kitaifa, katika kutatua kero za wafanyakazi kwa haraka.


Dini alieleza kuwa endapo Halmashauri ya wilaya hiyo, itaendelea kupuuza kero mbalimbali za wafanyakazi wake wilayani humo ni kuendelea kukuza migogoro mahali pa kazi isiyokuwa ya lazima, jambo ambalo litasababisha ufanisi wa kazi maofisini kushindwa kufikia malengo husika.

No comments: