Saturday, May 16, 2015

MADIWANI TUNDURU HAMASISHENI KUJIANDIKISHA KATIKA BVR

Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, limewataka viongozi wa serikali katika vijiji vya wilaya hiyo kutoa hamasa kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi, kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa kieletroniki (BVR).

Mwenyekiti wa baraza hilo la Madiwani la wilaya hiyo, Faridu Khamis alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza nao katika kikao walichoketi ukumbi wa Klasta ya walimu, tarafa ya Mlingoti mjini humo.

“Uhamasishaji wa wananchi waweze kujitokeza na kujiandikisha ni jambo la lazima ndugu zangu, jitahidini kuwahamasisha ili tuweze kufikia lengo husika”, alisisitiza.


Akizungumzia juu ya maendeleo ya zoezi hilo, Faridu alisema tayari kata kumi zilizopo kwenye tarafa ya Mlingoti limeonekana wananchi wake kuwa na hamasa wakijitokeza kwa wingi na kusababisha hata baadhi yao, kukimbilia vijiji jirani kwenye watu wachache ambao walijitokeza kujiandikisha.

Pia akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho ambapo katibu tawala wa wilaya hiyo, Ghaibu Lingo alifafanua kwa kuwataka wananchi waondokane na dhana kwamba kutakuwa tena na muda wa kuwaongezea kujiandikisha badala yake wanapaswa kulitekeleza hilo sasa, kwa kujitokeza kwa wingi na sio vinginevyo.


Jumla ya vituo 214 ambavyo vimegawanywa katika kata za wilaya hiyo, vimezingatia jiografia ya wilaya ambapo vituo 53 vinafanya kazi katika kata husika, kati ya mashine za BVR kit 74 zilizopokelewa.

No comments: