Thursday, May 7, 2015

MHOMA: WAANDISHI WA HABARI FUATENI MISINGI YA TAALUMA YA HABARI

Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imewataka waandishi wa habari kufuata misingi ya taaluma yao kwa kuandika habari zenye ukweli ili kuifanya nchi isiweze kuingia katika machafuko, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu.

Aidha imewataka kuwa watu wa kwanza katika kufichua vitendo vya rushwa, hatua ambayo itawawezesha wananchi wa kawaida kupata haki zao za msingi na kupenda kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Mapambano dhidi ya rushwa sio ya mtu mmoja, kila mtu anapaswa kushiriki kikamilifu ili kuifanya serikali ipate muda wa kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi wake ipasavyo”, alisema Ditram Mhoma.


Ditram Mhoma ambaye ni Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Mbinga, alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake katika mahojiano maalum, ambapo alikemea tabia za baadhi ya waandishi wa habari kuandika habari za upande mmoja ambazo hazina tija kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Kamanda huyo amewahimiza waandishi wa habari kuwa macho hasa wakati huu ambao taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, kwani kuna baadhi ya watu wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali hutumia waandishi kujisafisha hata kama hawana sifa ya kuwaongoza watanzania.

Pia amewataka kutokubali kugeuzwa kuwa wapiga debe wa wagombea hao, kwa kuandika habari za kuwapamba huku wakijua fika hawana sifa kwa kile alichoeleza kufanya hivyo kutawafanya wananchi waamini kinachoandikwa, na matokeo yake kujikuta wanaangukia mikononi mwa watu ambao hawana nia njema na taifa hili.


“Waandishi wa habari mna nafasi kubwa katika kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili uweze kwenda vizuri na pia mnaweza kuharibu, nawasihi angalieni namna mnavyoweza kutoa mchango wenu kikamilifu ili uchaguzi huu uweze kuwa huru na wenye utulivu”, alisisitiza Mhoma.

No comments: