Sunday, May 3, 2015

MKUU WA WILAYA TUNDURU AWAJIA JUU WANANCHI WAKE, AWATAKA KUZINGATIA USAFI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amewajia juu na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kujenga tabia ya kufanya usafi katika nyumba zao wanazoishi, ikiwa ni pamoja na kufua vyandarua vyao wanavyojifunika wakati wanapolala ili kuweza kuepukana na wadudu aina ya kunguni, ambao muda mwingi wamekuwa wakilalamika huwauma nyakati za usiku.

Aidha akatumia nafasi hiyo, kuwataka wananchi hao kupeleka watoto wao shule ili wakapate elimu ambayo itawawezesha kujitambua na kupambanua mambo, katika maisha yao ya kila siku na sio muda mwingi kuutumia kulalamika.

Hali hiyo imejitokeza kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu wilayani Tunduru, kujenga dhana ya kuendelea kulaumu serikali kwamba, imewasambazia vyandarua vyenye mayai ya kunguni na kusababisha kuwatesa hasa nyakati za usiku wanapokuwa wamelala.


Nalicho alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Njenga wilayani humo, kwenye maadhimisho ya mkutano wa Malaria Africa yaliyofanyika kiwilaya kijijini hapo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, mbali na serikali kuwaokoa wananchi wake wasiweze kushambuliwa na ugonjwa wa malaria, kwa kuwagawia vyandarua vya msaada bado wamejitokeza kwenye vyombo vya habari wakilalamika kwamba vina kunguni jambo ambalo sio la kweli, badala yake wanapaswa kuzingatia usafi majumbani kwao hasa sehemu wanayolala.


Pamoja na mambo mengine aliwataka watendaji wa wilaya hiyo, wakiwemo maafisa tarafa kupita vijijini kutoa elimu ya afya kwa wananchi wao, ili kuweza kuondoa malalamiko mengine ambayo hayana msingi wowote.

No comments: