Friday, May 1, 2015

WANANCHI TUNDURU WATAKIWA KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA MPIGA KURA

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akijiandikisha katika uzinduzi wa uandikishaji wa kitambulisho cha taifa katika kituo kilichopo kwenye ofisi za Mkuu huyo wa wilaya wilayani humo, kushoto kwake ni Afisa wa NIDA wilayani Tunduru. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewahimiza wananchi wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kupata vitambulisho vya kitaifa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo ambalo lilifanyika kwenye ofisi za mkuu huyo wa wilaya, zilizopo mjini hapa.

Nalicho alifafanua kuwa miongoni mwa faida za vitambulisho hivyo, ni pamoja na kila Mtanzania kutambuliwa kadhalika kitakuwa na msaada mkubwa kwa mtu binafsi hasa pale anaposafiri nje ya nchi.

Alisema kuwa wito huo ameutoa kwa wananchi wake wa wilaya hiyo, kutokana na kuwa pembezoni mpakani mwa Tanzania na Msumbiji hivyo kuwepo kwa vitambulisho hivyo kutasaidia hata mamlaka husika, kuwatofautisha wananchi wake kutokana na muingiliano uliopo miongoni mwao.


“Kitambulisho hiki ni muhimu sana, hasa kwa upande wetu wa Tanzania maana wenzetu nchi jirani ya Msumbiji tayari wao wamekwisha jiandikisha na kupatiwa”, alisema.

Awali akitoa taarifa za uanzishwaji wa zoezi hilo, Ofisa wa shirika la NIDA wilaya ya Tunduru Anafi Nachungu alisema kuwa shirika hilo litafanya zoezi hilo la utambuzi na usajili wa watu wilayani humo, kuanzia kwa watumishi wa serikali na baadaye kwa wananchi wa kawaida.

Zoezi hilo ambalo limeanza Aprili 24 mwaka huu, kwa kujaza fomu na kuchukua alama za vidole vya Mkuu huyo wa wilaya, limepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusuambao unatarajiwa kuishia mwanzoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.


Nachungu aliendelea kufafanua kuwa katika kipindi hicho, yeye na wasaidizi wake Dainas Mossy na Salvatory Majengo wamejipanga na kuhakikisha kuwa zoezi hili ambalo lilikwama kuanza mwezi Agosti 2014, linakamilika mapema na kwa wakati.

No comments: