Friday, May 22, 2015

FEDHA ZA KUNUNULIA BOTI ZILIZOTOLEWA NA WAZIRI MKUU PINDA WILAYANI NYASA ZAZUA MALALAMIKO

Wavuvi wakiwa katika ziwa Nyasa, wakitumia vifaa duni (mitumbwi) kuvulia samaki ambapo huhatarisha usalama wa maisha yao.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

VIKUNDI vinavyojishughulisha na uvuvi wa samaki Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, vimeutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuchukua hatua za haraka kufanya manunuzi ya boti la kisasa la kuvulia samaki, ambalo Ofisi ya Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda  alikwisha toa fedha kwa ajili ya kufanya manunuzi hayo.

Aidha wanakikundi hao ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini na hujishughulisha na shughuli za uvuvi katika ziwa Nyasa, walisema kuwa wanaushangaa uongozi wa wilaya hiyo tokea wapewe fedha shilingi milioni 14 na ofisi ya Waziri huyo, takribani miezi miwili imepita, hakuna majibu kamilifu waliyoyapata juu ya manunuzi ya boti hilo.

Walisema Waziri Pinda alitoa ahadi ya kununua chombo hicho cha kisasa kwa ajili ya kuwawezesha kuvua samaki kwa urahisi, alipokuwa hivi karibuni kwenye ziara yake ya kikazi wilayani humo baada ya kupokea kilio cha wavuvi hao kwamba wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuzama na mitumbwi majini, kutokana na kukosa kifaa cha kisasa cha kuvulia samaki.


“Ni muda mrefu sasa umepita hatujui kinachoendelea juu ya jambo hili, taarifa kamili tunayo kwamba tayari Waziri mkuu alikwisha leta fedha hizi alizoahidi kwa uongozi wetu wa halmashauri ili boti liweze kununuliwa, lakini kila tunapofanya ufuatiliaji kwa viongozi wetu wa wilaya hakuna majibu kamilifu tunayopewa”, walisema.

Vilevile utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, umebaini pia hata baadhi ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa nao wamekuwa wakilalamikia juu ya suala hilo, na kuutaka uongozi husika ambao hushughulikia manunuzi hayo kutekeleza suala hilo kwa haraka, ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa na msingi.

Madiwani hao walieleza kuwa fedha hizo za kununua boti, ofisi ya Waziri mkuu iliziwasilisha katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuzipeleka kwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nyasa, hatimaye taratibu za manunuzi ziweze kuendelea.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu ambapo alikiri kupokea fedha hizo na kuongeza kuwa zimekwisha pelekwa kwa uongozi wa wilaya hiyo, ili waweze kufanya manunuzi ya kifaa hicho cha kuvulia samaki.

“Ni kweli tumepokea fedha hizi na tayari tumekabidhi kwa uongozi wa Nyasa, naomba ufanye mawasiliano kwanza na Mkurugenzi wa Nyasa, atakupatia maelezo ya kina”, alisema Mwambungu.

Hata hivyo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Shaibu Nnunduma alithibitisha kupokea shilingi milioni 14 kwa ajili ya kununua boti hilo, huku akieleza kuwa wapo katika mchakato wa manunuzi hivyo wakati wowote kuanzia sasa taratibu husika zitakuwa zimekamilika na wanavikundi hao kukabidhiwa chombo hicho cha uvuvi.


No comments: