Saturday, May 16, 2015

FAMILIA WILAYANI TUNDURU YAOMBA MSAADA KUTOKA KWA WASAMARIA WEMA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

FAMILIA ya Athuman Mbwana, wa kijiji cha Nambalapi kata ya Masonya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma inawaomba wasamaria wema kutoa msaada wa kuwawezesha kulea watoto wao watatu, ambao walizaliwa kwa wakati mmoja ndani ya familia yao.

Mbwana alitoa ombi hilo, alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu baada ya wauguzi na wakunga wa Hospitali ya wilaya hiyo, kumtaarifu kuwa mkewe kipenzi Rehema Rashid ambaye alipelekwa hospitalini hapo akiwa mjamzito, kajifungua watoto hao kwa mpigo.

Aidha anaiomba serikali na taasisi binafsi kuwa na jicho la huruma, ili waweze kumsaidia kutunza watoto hao kutokana na yeye binafsi kuwa na kipato kidogo cha kumwezesha kuishi.

Alisema kupata watoto hao ni neema ya mwenyezi Mungu, na matokeo hayo hayakuwa matarajio yake hivyo anaomba msaada wa hali na mali ili aweze kuwatunza na kuwapatia mahitaji muhimu, ambayo yatawafanya waishi na kukua vizuri.


Naye Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta Mmari Zabron alithibitisha kuzaliwa kwa watoto hao watatu huku akiongeza kuwa Mama wa watoto hao alijifungua kwa njia ya upasuaji, watoto wakiwa na afya njema.

Mmari alifafanua kuwa mtoto wa kike wa kwanza kuzaliwa, alikuwa na uzito wa kilogramu 1.8 wa pili kilogramu 2.1 na mtoto wa mwisho ambaye alikuwa wa kiume alikuwa na uzito wa kilo 2.5.

Kadhalika alifafanua kuwa, watoto hao ambao kati yao walikuwa wa kike wawili na wa kiume mmoja baada ya kujiridhisha na maendeleo ya afya ya mama yao, uongozi wa Hospitali hiyo wakati wowote utamruhusu arejee makwao ili akaendelee na malezi ya familia yake.

Tunaomba kwa yule atakayeguswa na jambo hili, anaweza kutoa msaada wake kwa mawasiliano ya kupitia simu namba; 0786 041017 au 0689 595213.

No comments: