Sunday, May 10, 2015

NAMTUMBO WAJIVUNIA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA KUENDELEA VIZURI

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Alli Mpenye akizungumza katika kikao cha robo tatu ya mwaka baraza la Madiwani wa wilaya hiyo, kilichofanyika hivi karibuni mjini hapa. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Stephen Nana. (Picha na Muhidin Amri)
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

KATA tano zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, zimefanikiwa kuandikisha watu 30,832 katika daftari la kudumu la wapiga kura idadi ambayo imeelezwa kuwa ni moja kati ya mafanikio makubwa wakati zoezi hilo likiendelea kutekelezwa wilayani humo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Alli Mpenye alisema katika awamu ya kwanza zoezi hilo lilihusishwa katika kata tano za Mgombasi ambapo watu waliojiandikisha walikuwa 5,186, Namtumbo 9,041, Likuyu 4,952, Rwinga 7,586 na kata ya Luegu watu waliojiandikisha walikuwa 4,064.

Mpenye alifafanua kuwa hivi sasa wanaendelea na kata nyingine, na kwamba wamelazimika kufanya kwa wamu kutokana na ufinyu wa vifaa ikiwemo mashine ya kuandikishia wapiga kura (BVR) ambapo baadhi yake zilizoletwa na tume ya taifa ya uchaguzi ni mbovu na hushindwa kufanya kazi ipasavyo na kulazimika kutumia mashine chache zilizopo ambazo hufanya kazi.


Alieleza kuwa baada ya kumaliza kazi hiyo ya uandikishaji katika kata hizo, zoezi hilo litaendelea tena katika kata ambazo zipo pembezoni mwa wilaya hiyo ambazo ni Ligera, Lusewa, Mgazini na kata ya Msisima.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, awali kazi hiyo ilianza kwa kusuasua kwa kile alichoeleza kuwa mwitikio mdogo wa wananchi wenyewe na baada ya kuwafikia taarifa za kutosha katika maeneo yao, ndipo walianza kujitokeza kwa wingi.


Asasi za kiraia, wananchi na vyama vya siasa, Mpenye amevipongeza kwa jitihada yao ya kupita kuhamasisha zoezi hilo ili watu wakajiandikishe na ndio maana wengi wao hivi sasa katika vituo husika wilayani humo, wanahamasa kubwa ya kutekeleza zoezi hilo ili utakapofika uchaguzi mkuu ujao waweze kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemataka awaongoze, kwa nafasi ya Rais, Mbunge na Diwani.

No comments: