Saturday, May 9, 2015

NANA: MADIWANI NAMTUMBO ACHENI KUWA VIGEU GEU

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Stephen Nana, akifungua kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo ambapo aliwataka madiwani wake kuchapa kazi kwa bidii, sambamba na kusimamia maendeleo ya wilaya hiyo. Kushoto ni Makamu wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Khalifa Majumba.
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Stephen Nana amewataka Madiwani wa halmashauri hiyo kujifunga kibwebwe katika kusimamia mapato sambamba na ukusanyaji wa ushuru ipasavyo, ili kuifanya wilaya hiyo iweze kusonga mbele kimaendeleo.

Nana alitoa rai hiyo juzi, alipokuwa akifungua kikao cha robo mwaka cha baraza la madiwani hao huku akisisitiza muda wa kufanya kazi kwa mazoea umepita kilichobaki sasa ni kuhakikisha wananchi, wanapatiwa huduma za kijamii kwa wakati.

Alifafanua kuwa muda uliobaki kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ujao, ni vizuri kila diwani ajitathimini mwenyewe, namna alivyoleta mchango wa maendeleo kwa wananchi wake na wilaya kwa ujumla.


Kadhalika aliwataka kusimamia na kutekeleza maamuzi yote yanayofikiwa katika vikao husika, na kuacha tabia ya kuwa vigeu geu kwani kufanya hivyo kunaweza kurudisha nyuma mipango mbalimbali, inayofikiwa katika vikao hivyo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, baadhi ya Madiwani kutokana na kuwepo na tabia ya kujenga maslahi yao binafsi wamekuwa wakipindisha kwa makusudi sheria na kanuni zilizopo, kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe na kuiacha jamii ikiendelea kuteseka.

“Madiwani wenzangu ni lazima sasa tubadilike, hatutakiwi kuwa vigeu geu sisi ni watu wazima wananchi walituamini na kutuweka madarakani ni vizuri sasa safari hii tuliyoianza mwaka 2010, tuimalize tukiwa salama bila kuwepo malalamiko ya hapa na pale”, alisema Nana.


Pamoja na mambo mengine, watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo aliwataka kuacha tabia ya kulala usingizi sehemu ya kazi badala yake wajitume ili kuweza kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku, ili kuondoa umasikini uliokithiri katika wilaya hiyo.

No comments: