Monday, May 18, 2015

WAKULIMA WA KOROSHO WATAKIWA KUSAFISHA MASHAMBA YAO

Na Steven Augustino,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imeagiza na kuwataka wakulima wa korosho wilayani humo kuanza palizi mapema katika mashamba yao ya mikorosho, ili kuweza kuboresha zao hilo na kuzalishwa kwa wingi.

Faridu Khamis, ambaye ni Mwenyekiti wa halmshauri hiyo alitoa agizo hilo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni, ukumbi wa Klasta ya walimu mlingoti mjini hapa.

Khamis alisisitiza kuwa wakati wakulima hao, watakapokuwa wanafanya palizi katika mashamba yao waache vitendo vya uchomaji moto ambapo wakifanya hivyo, wanaweza wakasababisha mikorosho kuungua.


Alifafanua kwamba, hamasa hiyo anaitoa kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa wakulima wa zao hilo katika wilaya yake wamekwisha tengewa mgao wa tani 302,270 za madawa aina ya Sulpher duts, ambayo yatatumika kupulizia mikorosho yao.

Mgao huo utatolewa kutoka katika mfuko wa Wakfu, ambao unafanya kazi ya kuendeleza zao la korosho Tanzania (CIDTF) ambapo mpaka sasa umeweza kutenga lita 6,392 za madawa mbalimbali ya maji kwa ajili ya kupulizia zao hilo.

Awali akitolea taarifa ya ujio wa madawa hayo Mwenyekiti wa mfuko huo, Athuman Nkinde alieleza kuwa madawa hayo yatafikishwa kwa wakulima husika wilayani humo mwishoni mwa mwezi huu.

Nkinde alisema madawa yote yatafikishwa katika ofisi za vyama vya ushirika wilayani Tunduru, na kwamba yatauzwa kwa bei husika ya ruzuku ambayo imepangwa na mfuko.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mfuko mmoja wa Sulpher duts ambao una ujazo wa kilo 25 utauzwa kwa shilingi 15,000 badala ya 45,000 ambayo huuzwa na walanguzi, kitendo ambacho humuumiza mkulima na kumfanya aendelee kuwa maskini.


Alisema lengo la mfuko kuweka bei hiyo ni kumkomboa mkulima huyo mwenye kipato cha chini, na kwamba mgao wa pembejeo hutolewa kwa kuzingatia uzalishaji wa korosho ambapo katika msimu wa mwaka 2014/2015 wilaya hiyo, ilipewa mgao wa kilo 7,452,339.

No comments: