Friday, May 29, 2015

MARIO MILLINGA KUPAMBANA NA GAUDENCE KAYOMBO

Mario Millinga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mario Millinga ametangaza nia yake ya kutaka kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma ambalo hivi sasa linaongozwa na Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gaudence Kayombo.

Kada huyo wa CHADEMA alisema kuwa ameshawishika kugombea nafasi hiyo ili wananchi wa wilaya hiyo, waone jinsi uongozi wa chama chake unavyojali maslahi ya wananchi hasa kwa wale waishio vijijini ambao muda mwingi, wamekuwa wakisahulika katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

“Ubunge ni uwakilishi wa wananchi katika eneo husika, tunapomchagua mbunge au diwani ambaye si mkazi wa eneo la uwakilishi tunajitwika mzigo wa shida sisi wenyewe, ndugu zangu mimi ni mzaliwa wa kijiji cha Tukuzi hapa Mbinga nimedhamiria kugombea katika nafasi hii, ili niweze kuwatumikia ipasavyo wananchi wa jimbo hili”, alisema Mario.

Mario alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juu ya nia yake ya kutaka kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania nafasi ya ubunge, jimbo la Mbinga Mashariki na kwamba ni kijana na kada wa siku nyingi wa chama hicho ambaye amebobea katika masomo ya biashara, uhasibu na uchumi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya mlimani na kuhitimu elimu ya biashara ngazi ya Bachelor of Education in Commerce.


Alisema kuwa amefikia hatua ya kutekeleza hilo, baada ya kuona chaguzi mbalimbali zilizopita wilaya imekuwa ikitawaliwa na wabunge wa kutoka nje jambo ambalo uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, wanambinga wameweka mkakati wa kutaka kuongozwa na mzawa ambaye amezaliwa katika wilaya yao na sio vinginevyo.

 Pamoja na mambo mengine alifafanua kuwa CHADEMA katika wilaya ya Mbinga hivi karibuni imefanya ziara yake ya kikazi mjini na vijijini, kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, ili muda wa uchaguzi utakapowadia wananchi waweze kufanya mabadiliko ya kweli.

Alifafanua kuwa baadhi ya viongozi wa kitaifa kutoka katika chama hicho amekuwa akiambatana nao katika ziara hiyo, pamoja na timu nzima ya sanaa ambayo ilikuwa ikiongozwa na mwimbaji mashuhuri Mwanakotide ambao walikuwa wakizunguka katika kata za wilaya hiyo, kuendesha mikutano ya kuelimisha wananchi kujiandikisha katika daftari hilo.

“Kufuatia mikutano hii tuliyoifanya ninyi wenyewe mtakuwa mashahidi wananchi wengi vijijini na mjini wamehamasika juu ya kujiandikisha, dhana ya CCM kudanganya watu kwamba wapinzani ni watu wakuleta vurugu sasa imepitwa na tukiwasikia wanayasema haya tuwapuuze”, alisema.

Hata hivyo aliongeza kuwa kiongozi mzuri anatakiwa kujali maslahi ya wananchi wake waweze kuishi kwa amani na utulivu, ikiwemo kufanya shughuli zao kwa furaha na kwamba yeye binafsi endapo wananchi wa Mbinga watampatia ridhaa ya kuwaongoza atahakikisha anakabiliana na kero mbalimbali, ambazo zimekuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu hususani katika nyanja ya kimaendeleo.

No comments: