Tuesday, May 19, 2015

MAOFISA UGANI RUVUMA WAJENGEWA UWEZO

Na Julius Konala,
Songea.

MAOFISA ugani katika Halmashauri nne zilizopo mkoani Ruvuma, wameweza kujengewa uwezo juu ya matumizi sahihi, katika tekinolojia mpya ya uhifadhi wa mazao.

Lengo la maofisa hao kupewa elimu hiyo, ni kuwataka katika maeneo ambayo wanafanyia kazi mkoani humo, waende kwa wakulima vijijini wakawaelimisha juu ya tekinolojia hiyo na baadaye waweze kuhifadhi mazao yao katika hali nzuri.

Mafunzo juu ya matumizi sahihi ya uhifadhi wa mazao, yalifanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano Walimu SACCOS mjini Songea, ambayo yalikuwa yakiendeshwa na shirika la CARITAS na CRS.

Jumla ya maofisa ugani 32 kutoka wilaya ya Songea, Namtumbo, Mbinga na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameweza kupata elimu hiyo.

Mwakilishi mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Georgina Mbawala alisema washiriki hao mara baada ya kumaliza kupewa mafunzo hayo watakuwa walimu wazuri, katika suala la uhifadhi huo ambao unalenga kuhifadhi mazao katika kipindi cha miaka mitatu bila ya kushambuliwa na wadudu waharibifu.


Naye Ofisa mradi kutoka katika shirika hilo PICS CARITAS jimbo kuu la Songea, Brito Mgaye amewataka wakulima kutumia tekinolojia hiyo watayopewa na maofisa hao wa ugani, ili kupunguza upotevu wa mazao yao mara baada ya mavuno shambani pamoja na kuwapunguzia gharama ya ununuzi wa madawa ya kilimo ambayo hutumika kupulizia wakati wa kuhifadhi mazao katika maghala.

Alisema kuwa asilimia 50 ya mazao ya wakulima hupotea kwa kushambuliwa na wadudu waharibifu, kutokana na wengi wao kutokuwa na tekinolojia ya kisasa juu ya uhifadhi wa mazao yao.


Wakuu wa wilaya na wakurugenzi mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuipokea tekinolojia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa wakulima itawaondolea adha kubwa katika kuhifadhi mazao yao, na kuwafanya waweze kukuza uchumi wao.

No comments: