Friday, May 29, 2015

MGAWANYO WA MAJIMBO YA UCHAGUZI MBINGA WAZUA MALALAMIKO

Kaimu Mkurugenzi wa uchaguzi Kailima R.K akizungumza hivi karibuni na vyombo vya habari hapa nchini, kuhusu uchunguzi wa mipaka na kugawa majimbo kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu, katika ofisi za makao ya tume ya uchaguzi.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

PENDEKEZO la kuligawa Jimbo la Mbinga Mashariki, lililopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma limeingia dosari kufuatia kuwepo kwa malalamiko yanayodaiwa kwamba mchakato huo wa kuligawa jimbo hilo, umefanywa na viongozi wachache bila kushirikisha wadau mbalimbali wa wilaya hiyo, kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni ukiukwaji wa maagizo na taratibu zilizotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi hapa nchini.

Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, walitoa malalamiko hayo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti huku wakiitaka serikali kuwa makini na suala hilo ambalo kutokana na wadau husika kutoshirikishwa kama vile taratibu za tume katika kurekebisha mipaka, kugawa majimbo na kubadili majina zinavyotaka.

Mapendekezo hayo ya kuligawa jimbo hilo yamefanyika muda wa nusu saa katika kikao cha dharula cha baraza la madiwani, kilichoketi Mei 27 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Hata baadhi ya Madiwani ambao walikuwepo katika kikao hicho nao walionesha kushangazwa na hali hiyo, wakisema kuwa walitumiwa ujumbe kwa njia ya simu kwamba wanatakiwa katika kikao cha dharula kwa tarehe hiyo, bila kufafanuliwa kinahusu nini na walipowasili walikutana na ajenda hiyo ya pendekezo la kuligawa jimbo. 


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa takwimu za wilaya ya Mbinga kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 385,354 idadi ambayo haitoshelezi katika kufanya mgawanyo wa watu kwa majimbo mawili.

Vigezo na taratibu zilizotolewa na tume ya uchaguzi Mei 10 mwaka huu, ambazo nakala yake tunayo inaagiza kuwa vitatumika katika kuchunguza mipaka na kugawa majimbo kwa uchaguzi wa wabunge, huku mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu (Population quota) unapaswa kuzingatiwa.

Jimbo la Mbinga mashariki ambalo kwa sasa limetolewa pendekezo la kuligawa majimbo mawili, la Mbinga mjini lenye idadi ya watu 129,537 na vijijini kuna watu 255,817 idadi ambayo imefafanuliwa kuwa ni ya watu wachache katika kufanya mgawanyo wa majimbo hayo.

Kadhalika mkazi mmoja wa kata ya Matarawe Mbinga mjini, Hamis Nanyanje akizungumzia hilo alisema kuwa mchakato huo wa kuligawa jimbo la Mbinga Mashariki kuwa majimbo mawili kwa sasa ni mapema mno, sawa na kuitwisha serikali mzigo mzito pasipo sababu ya msingi kwa kile alichodai kuwa kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya watu, katika wilaya hiyo.

Naye Astery Ndunguru alifafanua kwamba itakuwa ni jambo la kushangaza endapo mgawanyo huo serikali itaridhia huku akitolea mfano, hata kwa Manispaa ya Songea ambayo idadi yake ya watu ni kubwa hawana majimbo mawili, hivyo alihoji inawezekanaje kwa wilaya ya Mbinga ambayo idadi yake ya watu ni ndogo igawanywe kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi ?.

“Majimbo ya uchaguzi yanayostahili kuwasilisha maombi kwa mujibu wa utaratibu ulioainishwa na tume ni yale yenye idadi kubwa ya watu wasiopungua 325,000 kwa majimbo ya mjini na watu 235,000 kwa majimbo ya vijijini”, alisema Ndunguru.

Cosmas Haulle mkazi wa kata ya Maguu alibainisha kuwa katika mgawanyo huo tume ya uchaguzi imekuwa ikizingatia pia suala la upatikanaji duni wa mawasiliano katika eneo husika kama vile barabara, simu, redio na magazeti vimekuwa vikipewa kipaumbele ambapo kwa wilaya hiyo mawasiliano hayo yamekuwa yakipatikana kwa urahisi kuliko kwenye maeneo mengine.


Hata hivyo alipohojiwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga juu ya malalamiko hayo ya wadau mbalimbali kutoshirikishwa katika kikao hicho cha mapendekezo ya mgawanyo huo wa majimbo alisema; “mimi nipo safarini sijui huo mchakato huko umeendeleaje, hayo malalamiko ambayo wadau wamekuletea naomba uyapuuze, huenda walipewa taarifa kwa njia ya barua wao hawakufika na haiwezekani sisi tushindwe kupitisha mchakato huu kwa sababu suala hili lilikuwa na uharaka”, alisema Ngaga.

No comments: