Thursday, May 7, 2015

WAKULIMA NAMTUMBO WANUFAIKA NA TEKINOLOJIA YA KILIMO CHA KISASA

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ally Mpenye wa pili kutoka kushoto akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wakulima wa zao la mpunga wilayani humo, Gerold Haulle ambaye amevaa kofia kushoto kwake katika moja ya shamba darasa la majaribio kilimo cha zao hilo. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa taasisi ya Briten nyanda za juu Kusini, Ainea Mgulambwa. 
Na Julius Konala,
Namtumbo.

WAKULIMA wanaozalisha zao la mpunga wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wamenufaika na elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na upandaji wa zao hilo katika mashamba darasa, yanayoendeshwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Briten kupitia ufadhili wa shirika la kuleta mapinduzi ya kijani barani Afrika, AGRA.

Zaidi ya wakulima 2,660 ndio walionufaika na mpango huo, ambapo Mratibu wa kitengo cha shamba darasa na mtaalamu wa kilimo cha zao la mpunga wilayani humo, Saamy Mwakyusa alisema hayo kwenye uzinduzi wa siku ya mkulima kiwilaya iliyofanyika kijiji cha Namtumbo mbele ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Ally Mpenye.

Mwakyusa alisema kuwa, elimu hiyo ambayo wameipata wakulima wake imeleta tija kwa madai kwamba jumla ya mashamba darasa 76 katika vijiji vya wilaya hiyo, vimeonyesha kufanya vizuri na wakulima wengi wamepata mafunzo ya kilimo hifadhi ya udongo.


Mmoja wa wakulima bora kutoka katika kijiji cha Namtumbo, Gerold Haulle aliipongeza taaisisi ya Briten kwa kuwapa elimu hiyo pia yakiwemo na mafunzo ya mawakala wa usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima, ambapo kufanya hivyo kumeweza kusaidia kuongeza uzalishaji na kipato kwa ngazi ya familia.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Ally Mpenye alipongeza jitihada hizo ikiwemo na benki ya CRDB kwa kuwawezesha wakulima hao, kuwapatia tekinolojia ya kilimo bora na cha kisasa.

Aidha Mpenye aliwaasa wakulima kusindika mazao yao katika ubora na usalama, kwa lengo la kukabiliana na ukosefu wa masoko pamoja na walanguzi ambao wamekuwa wakiwanyonya kwa kununua mazao kwa bei ya chini na kumfanya mkulima, kushindwa kunufaika huku akiendelea kubaki katika hali ya umaskini.

Pamoja na mambo mengine Mratibu wa Briten nyanda za juu Kusini, Ainea Mgulambwa alifafanua kuwa lengo kuu la mradi huo ni kusambaza tekinolojia ya kilimo bora kwa wakulima, ili waweze kuongeza uzalishaji na kipato katika maisha yao na kwamba taasisi hiyo imekwisha fanikiwa kufikisha tekinolojia husika katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo wilaya ya Ludewa, Kilolo, Songea na Namtumbo.


No comments: