Sunday, May 3, 2015

WANAOTAFUTA MADARAKA KWA MTINDO WA RUSHWA, TUWABEZE

Na Mwandishi wetu,

TUMEONA na tutazidi kuona wanaotangaza nia ya kuwania nyadhifa mbalimbali, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015 kuna mengi yamejitokeza na bado yataendelea kujitokeza hivyo ni vyema tukayajadili kwa mapana kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na hata nafasi ya urais.

Napenda kuhoji, je hao wanaotangaza nia wanatangaza nia kweli au ni dhidi ya rushwa? kwa hali ya kawaida katika jamii yetu ya kitanzania imegubikwa na wimbi la rushwa, hivyo msamiati huu umekuwa ni wa kawaida hivyo hata mtu ukimtuhumu ni mlarushwa inaonekana ni jambo la kawaida.

Hivyo wengi wametegwa na rushwa, sitakosea nikisema mifumo yetu imekuwa lege lege dhidi ya kupambana na vita ya rushwa tena hata ufisadi.

Wakati tukiyasemea haya hivi sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, huko ndiko tunakotarajia kuwapata viongozi watakao tuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, endapo tutacheza karata nzuri nina hakika tutaweza kuwapata viongozi waadilifu na pia endapo tutacheza vibaya tutaishia kupata viongozi ambao sio waadilifu hivyo karata zetu, zitakuwa ni shida na mateso makubwa katika kipindi hicho cha miaka mitano.


Wapo tulionamashaka nao, wapo tusiowajua na wapo tunaowajua kwa undani na wenye uadilifu, hivyo bado tuna safari ndefu ya kuwapima na kuchukua maamuzi sahihi na yenye kuweza kutuongoza.

Wapo waliofanya vizuri na waliofanya vibaya hivyo wote tunawatambua, vilevile tunataka kuwaangusha walio waadilifu na pia wapo wanaotaka kuwaangusha wasio waadilifu, katika hili nasema wote kwa sasa ni watangaza nia tu.

Napata shida sana ninapoona, wanaotangaza nia kwa kuangalia mienendo yao iwe ni wale waliokwisha onyesha uwezo wao au wanaotangaza nia ya kurithi nafasi za udiwani, ubunge na hata urais?

Sijasikia kwa uwazi waliotangaza nia dhidi ya rushwa, ila nasikia minong’ono ya rushwa tena kwa makundi ya wapambe yakiwa tayari kutumia rasilimali watu na fedha, kuhakikisha tu yanafikia malengo yao waliyojiwekea.

Wapo waliojipanga kuwapigia chapuo wagombea wenye ukwasi na wengine wamejipanga kuona viongozi waadilifu, wakipata nafasi ya kutuongoza lakini vita kubwa dhidi ya rushwa sasa imekuwa butu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa pamoja na mifumo ya sheria na kitaasisi inayofanya kazi ya kuidhibiti kuwa lege lege?

Je, kwa eneo ulilopo ni nani hasa ametangaza nia huku ajenda yake ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na ufisadi?, ni mikakati gani ameibuni ili kudhibiti rushwa na ufisadi?, Je ni wangapi wametangaza nia juu ya kupambana na adui huyu?................ katika hili natambua majibu tunayo wenyewe.

Je, kwa namna gani unamwona mgombea kama kielelezo cha vita dhidi ya ufisadi, ni sahihi kumpigia kampeni mtu usiyemjua vizuri kwa sababu tu una maslahi yako binafsi?

Nyie wagombea mnao tutangazia nia hapa nchini katika kila mikoa na wilaya zake, mnaweza mkaweka wasifu wenu wazi hasa uadilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi?

Ni mikakati gani mliyonayo mtakayoiweka ili kupambana na rushwa na ufisadi? wapo wengine mna kashfa za ufisadi na rushwa je hamuoni nyie ni kikwazo cha vita dhidi ya rushwa na ufisadi? je ni kitu gani mnatuambia dhidi ya kashfa zinazowakabili?

Wapambe na wagombea ambako kila kukicha mnawaza kutoa rushwa mnataka nini baada ya yule mnayempa “Saport” kupata uongozi, hivi kweli atawajali wananchi waliompa kura kwa rushwa?

Je, hivi mnashindwa kujua tofauti iliyopo kati ya kiongozi bora na bora kiongozi, Je, mnashinda kutwa nzima kutuaminisha sifa za mgombea au  wagombea wenu hamuoni huu ni unafiki na usaliti dhidi ya taifa?

Umaskini umekithiri, huduma kwa jamii ni hafifu lakini bado tunawaza kuwapigia chapuo viongozi wasio waadilifu, migogoro ndani ya jamii inaibuka kila kukicha, chanzo chake ni kukosa uadilifu kwa viongozi wetu katika kuwaongoza wananchi.

Kadhalika nao uhasama unakua kila kukicha, rushwa na ufisadi umechukua nafasi lakini bado tunawaza kuhonga  fedha na pombe kipindi cha uchaguzi, ili tuwachague wasio waadilifu na kuendelea kuitesa jamii, sitakosea nikisema yatupasa sasa tubadilike.

Hizi ni zama za uwazi na ukweli, haya yote mamlaka zilizopo zinayajua lakini hazichukui hatua, ni nani sasa kati yetu achukue hatua, wengi wananong’ona pale wanapohojiwa uadilifu wao.

Linapofika suala la uwajibikaji ni kiburi, utadhani ni haki yao kupora mali ya umma wapo tayari hata kurubuni baadhi ya watu ilimradi tu wajisafishe ndani ya jamii, hivi kweli tunawapima viongozi wetu uadilifu wao kabla hatujawachagua?

Ushauri wangu kama ndani ya kata yako au jimbo lako mliweza kupata kiongozi mwadilifu ni vyema mkamchagua mwadilifu. 

Pia kama mlimpata mgombea asiye mwadilifu ni vyema mkatafuta aliyetangaza nia dhidi ya rushwa hakika akisimama semeni, huyu ndiye mgombea pekee na atatufaa kuwa kiongozi imara hivyo tusifanye makosa.

Hivi viongozi wa vyama vya siasa, wamejiandaa vipi kupambana na changamoto hii ya rushwa ndani ya vyama vyao wakati wakuwapata wagombea? Je, wamejipanga vipi kuwadhibiti wagombea watakaotoa rushwa?

Au wapo tayari kuona wagombea wao wakikaa katika nafasi za uongozi, kwa jitihada yoyote ile hata kwa matumizi ya kugawa fedha chafu kila kona? upi ni mustakabali wa wagombea wao na maslahi kwa taifa hili, endapo wanatumia rushwa na hawadhibitiwi.

Pia katika hili tusifungwe na fikra mgando ambazo zimejengwa kwa misingi ya itikadi za vyama vya siasa, dini, kabila, urafiki au uswahiba maana huo ndio utakuwa mwanya wa rushwa na ufisadi ndani ya jamii pia utakuwa ni kikwazo kikubwa, katika kumpata mgombea mwadilifu ndani ya chama na pia kumpata kiongozi bora atakaye tuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Hivyo katika harakati za kumpata kiongozi tusiende kwa hila na chuki dhidi ya propaganda chafu, dhidi ya washindani wetu na pia uungwana utumike pale tunapoona yupo anayeweza kutuongoza.

Ni vyema sasa tumpatie nafasi ili atuongoze kwa manufaa yetu wote, kadhalika tuwakane wazi wazi wasiofaa, watoa rushwa na hata wapambe wao na wachukuliwe hatua stahiki pale wanapobainika.

Pia tuwaepuke wagombea na wapambe kwa nafasi yoyote ile, kuanzia ndani ya chama na hata nje ya chama ambaye dhahiri amejikita katika kununua uongozi, ni imani yangu hafai na kamwe tutakuwa tumechagua chaguo lisilo sahihi kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu, hivyo tujihadhari na watangaza nia wanaotumia mwanya wa rushwa kupata madaraka, tuwatofautishe na tuwabaini sifa zao na baadaye tuseme Yes or No.


Hitimisho langu ni kwamba, tukifeli katika mchakato huu kwa vigingi vya rushwa, propaganda na siasa chafu tusitarajie kupata matokeo mazuri, hakuna chema kitakachotokana na mfumo mchafu ili uzalishe matokeo mazuri hivyo tujihadhari katika mchakato wa uchaguzi, na pia katika mchakato wa kuipata katiba mpya yatupasa tuzingatie hili.

No comments: