Saturday, May 16, 2015

DIWANI MBINGA ADAIWA KUNYANYASA WAPIGA KURA WAKE, ATUHUMIWA KUTUMIA MADARAKA YAKE VIBAYA

Vibanda vya nyasi ambavyo wanaishi baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ilela, ambao waliyakimbia makazi yao baada ya kuogopa kukamatwa na askari polisi wa kituo kidogo cha Maguu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa shinikizo la kuwataka wakaishi katika kijiji cha Ugogo wilayani humo. 

Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Ilela wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuishi porini wakiwa katika makazi yao mapya kama wanavyoonekana pichani. 
Na Muhidin Amri,
Mbinga.

ZAIDI ya watu 200 waishio katika kijiji cha Ilela kata ya Mikalanga wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamehama makazi yao na kulazimika kuishi porini kwa kile walichoeleza kuwa wanaepuka kukamatwa, kuwekwa mahabusu na kuteswa na askari Polisi wa kituo kidogo cha Maguu wilayani humo ambao wanalazimisha kutoa michango ya fedha, kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha polisi katika kata hiyo.

Mbali na hilo watoto chini ya miaka mitano wanashindwa kupata huduma ya matibabu ya kliniki, baada ya uongozi wa kijiji hicho kudaiwa kuandika barua kwenda uongozi wa zahanati ya Ilela ikizuia watoto wenye wazazi ambao wamekimbilia porini, wasipatiwe huduma ya matibabu.

Akina mama nao imefikia hatua sasa, hulazimika kutembea umbali wa kilometa tisa kwenda katika kijiji cha Burma, kufuata huduma hiyo ya matibabu kwa watoto wao.

Kufuatia hali hiyo, pia wanamtuhumu Diwani wao wa kata hiyo Joachimu Kowelo kwa kitendo chake cha kuwagawa wananchi wa kata hiyo kwa kuuagiza uongozi wa kijiji na kata kuwahamisha kwa nguvu baadhi ya wananchi wake, wakaishi kijiji kipya cha Ugogo kwa maslahi yake binafsi kitendo ambacho kimefafanuliwa kuwa ni cha kinyama.


Wakazi hao waliendelea kueleza kuwa, wamelazimika kuhama katika nyumba zao na kukimbilia kuishi porini kwa lengo la kuepuka manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa askari hao Polisi wa kituo cha Maguu, ambao huvamia makazi yao nyakati za usiku na kulazimisha wananchi watoe michango.

Walieleza kuwa kila siku wamekuwa wakiishi kwa taabu, huku wakikesha usiku kucha kuwakimbia askari hao ambao hufika nyakati za usiku wakiwakamata na kuwaweka mahabusu, na kuwatoza shilingi 45,000 kama dhamana na shilingi 87,000 kwa ajili ya uendeshaji wa kazi za polisi jambo ambalo ni la uonevu na la kusikitisha.

Kwa mujibu wa maelezo ya wakazi hao wameendelea kumnyoshea kidole Diwani wao Kowelo, wakisema ndio chanzo cha hayo matatizo wakidai kuwa ameapa kuwashughulikia watu wote wanaompinga katika harakati za kutaka kurudi tena madarakani katika kugombea, kwenye nafasi hiyo ya udiwani.

Veronica Mbele, Edwin Nombo, Suzy Mahayi na Menas Nombo walisema kwa nyakati tofauti diwani wao ndiye aliyeshinikiza kwa uongozi wa kijiji na kata ili wahamie katika kijiji cha Ugogo na kuwatumia askari hao wawaletee usumbufu, ikiwemo kuwafungulia hata mashtaka ambayo hayana ukweli huku wengine wakiapa kwamba wapo tayari kufia katika kijiji cha Ilela, na sio huko ambako wanalazimishwa wahamie.

Walisema wao wanahitaji kuendelea kuishi katika kijiji hicho, kwani hakuna sababu ya msingi ya wao kupelekwa huko licha ya serikali kukigawa kijiji cha Ilela na kuzaliwa kijiji cha Ugogo, huku wakiongeza kuwa hawana ulazima wao kwenda kijiji hicho kipya kwani tayari wana makazi ya kudumu katika kijiji cha Ilela na ambako wanapata huduma za maji na tiba.

Angelus Komba, naye alisema licha ya kijiji cha Ugogo kuundwa kisheria hakuna sababu ya kulazimisha watu wakaishi huko, badala yake ni vyema ukafanyika utaratibu wa kukaa na wananchi husika kwa kufanya kikao cha pamoja cha maradhiano, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa badala yake diwani ndiye anayeonekana kufanya mambo hayo ya kipuuzi ya kutesa wapiga kura wake, hasa kwa mtu ambaye anampinga katika shughuli zake za kiutawala.

Diwani wa kata ya Mikalanga, Joachimu Kowelo alikana kuhusika na tuhuma hizo ambapo alieleza kwamba wananchi hao hawakupaswa kuyakimbia makazi yao.

“Hawa wananchi ni wapuuzi sana, mimi binafsi nashindwa kuwaelewa ni sababu gani ya msingi iliyowafanya wayakimbie makazi yao na kwenda kuishi porini, hizi najua ni njama za kisiasa tu”, alisema Kowelo.


Hata hivyo jitihada ya kumpata Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya tuhuma wanazotuhumiwa askari wake ziligonga mwamba na simu yake, ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: