Sunday, May 24, 2015

DEREVA AFARIKI DUNIA FUVU LA KICHWA LAPASUKA BAADA YA KUPATA AJALI KONA YA MBWA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

DEREVA mmoja ambaye amekuwa akiendesha magari makubwa ya mizigo na hufanya safari zake katika maeneo mbalimbali hapa nchini, amefariki dunia katika ajali iliyotokea kona ya mbwa eneo la Nakayaya, karibu na kiwanda cha kubangua korosho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Said Jiram (37) ndiye aliyefariki dunia ambapo ndani ya gari alilokuwa akiliendesha lenye namba za usajili T 481 ATZ aina ya Toyota Carina ambalo ndani yake alikuwa na wenzake wawili, ambao walinusurika kifo.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walieleza kuwa watu hao walipatwa na mkasa huo wakati walipokuwa wakielekea karibu na kiwanda hicho, kwa lengo la kwenda kupakia korosho kwenye lori hatimaye wasafirishe kwenda Jijini Dar es Salaam.

Akifafanua juu ya tukio hilo rafiki wa marehemu huyo, Mohamed Mponda ambaye ni mmoja aliyenusurika kwenye ajali hiyo alisema kuwa yeye na marehemu walikuwa pamoja kwenye gari hilo, ambapo wakiwa njiani kuelekea huko ghafla gari lilipinduka mara mbili na kusababisha kifo kutokana na Jiram kupatwa na majeraha mengi mwilini huku akitokwa na damu nyingi.


Mohamed alifafanua kuwa baada ya tukio hilo aliomba msaada wa gari kwa kampuni ya Kichina (CCECC) ambayo ipo katika barabara hiyo ya Tunduru, ikifanya kazi ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ambapo walimkimbiza katika hospitali ya wilaya, kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Walipofika hospitalini hapo licha ya matabibu kufanya jitihada ya kuokoa uhai wake hawakufanikiwa, ambapo alikata roho muda mfupi wakati akiwa mikononi mwao wakiendelea kumpatia matibabu.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kilisababishwa na mwendo kasi, hali ambayo ilisababisha marehemu kushindwa kumudu gari hilo na kumfanya kuyumba nalo kukosa mwelekeo kisha kupinduka.


Hata hivyo Mganga aliyeufanyia mwili wa marehemu Jiram, Dokta Andreas Ndunguru alisema kifo hicho kilitokana na kutokwa na damu nyingi baada ya kupata mpasuko wa ndani kwa ndani, katika fuvu la kichwa chake.

No comments: