Monday, May 4, 2015

WAIOMBA SERIKALI WASAIDIWE MADAKTARI BINGWA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupeleka Madaktari bingwa katika Hospitali za mikoa ili kuwasogezea huduma ya afya kwa karibu, kutokana na wengi wao kusumbuliwa na magonjwa sugu na kushindwa kumudu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika hospitali za rufaa.

Kauli hiyo ilitolewa na wananchi hao, walipokuwa wakipatiwa huduma ya matibabu na madaktari bingwa waliowasili katika hospitali ya serikali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali ikiwa ni lengo la kuongeza nguvu ya utoaji wa huduma ya matibabu katika hospitali hiyo.

Madaktari hao waliwasili hapo wakitokea hospitali mbalimbali Jijini Dar es salaam, KCMC Moshi na kwamba wananchi wa wilaya ya Tunduru walishukuru kwa ujio wao hasa kwa wale ambao walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa kwa muda mrefu, bila kupatiwa matibabu ya kudumu.


Msewe Athuman na Asha Likambale ni baadhi ya wananchi waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi na kupata fursa ya kutoa maombi hayo kwa serikali yao, ili waweze kuondokana na adha hiyo kutokana na hospitali za rufaa kuwa mbali nao na kusababisha wananchi wengi kupoteza maisha.

Walisema kutokana na hali yao ya maisha kuwa ngumu, wengi wao wamekuwa wakipata hata ulemavu wa maisha kutokana na kukosa matibabu husika.

Kwa upande wake akizungumzia ujio wa Madaktari hao, Mganga mkuu wa wa wilaya ya Tunduru, Dokta Alex Kazula alisema kwamba wazo la kuwaleta wataalamu hao lilitokana na idara yake kutambua uwepo wa mahitaji makubwa ya matibabu, kutokana na wananchi wa wilaya hiyo kusumbuliwa na magonjwa sugu kwa muda mrefu.

Dokta Kazula alifafanua kuwa wataalamu hao ni mabingwa wa magonjwa ya upasuaji na ya wanawake na wamepelekwa katika wilaya hiyo, kutokana na wananchi wake kuwa pembezoni mpakani mwa nchi ya Tanzania na Msumbiji.

Alisema kuwa idara yake inawajali wananchi hao na ndio maana imeleta madaktari hao, ambapo mpango huo ulianzishwa tokea mwaka 2014 wa kuwaleta kila mwaka ili wagonjwa wenye magonjwa sugu, waweze kupatiwa matibabu.

“Mpaka sasa huduma ya upasuaji mkubwa kwa magonjwa sugu wamefanyiwa wagonjwa 26, elimu ya afya imetolewa pia kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kawaida zaidi ya 137”, alisema Dokta Kazula.

Pamoja na mambo mengine, Dokta Kazula aliongeza kwa kuwaomba wafadhili kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuleta madaktari kama hao ili kuweza kutoa huduma ya matibabu, kwa wananchi wengi zaidi.

Kikundi cha Madaktari hao ambacho kinaundwa na kundi la JITOLEE, kina madaktari 20 huzunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kutoa huduma ya matibabu kwa lengo la kuokoa maisha ya Watanzania wenzao.


Dokta Erick Mulumba alibainisha kuwa kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2014, tayari kimefanikiwa kuokoa maisha ya wananchi 137 kati ya 147waliofanyiwa upasuaji mkubwa katika wilaya ya Tunduru, Lindi, Lwangwa na Muheza.

No comments: