Saturday, August 16, 2014

WALEMAVU NAMTUMBO WAPATIWA MAFUNZO YA KUTAMBUA HAKI ZAO

Na Kassian Nyandindi,


Namtumbo.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la kuendeleza watu wenye ulemavu na watoto yatima Tanzania (SHIKUWATA) lenye makao yake makuu mkoani Ruvuma, limeendesha mafunzo ya siku tano kwa watu wenye ulemavu na Watendaji wa kata ya Namabengo Wilayani Namtumbo mkoani humo, kwa lengo la kuwafundisha juu ya kujua sera ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu.

Mafunzo hayo ambayo yalifunguliwa na Diwani wa kata ya Namabengo wilayani humo Vitus Ngonyani, ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Namabengo Saccos uliopo mjini hapa na kushirikisha wananchi mbalimbali wanaoishi kuzunguka eneo la kata hiyo.

Mratibu wa shirika hilo Laura Martin akizungumza katika mafunzo hayo, alisema kuwa lengo la kutoa elimu kwa walemavu hao ni kuwafanya wajue haki zao na wajibu wa kujihudumia pamoja na kuangalia nafasi waliyonayo katika jamii na serikali kwa ujumla.

Laura alisema kuwa washiriki hao katika kipindi chote cha siku tano watakachokuwa darasani wataweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kujua hali ya watu wenye ulemavu, huduma za watu wenye ulemavu, haki na ulinzi wa kisheria, dira na mwelekeo wa sera, matamko ya sera kwa watu wenye ulemavu na mgawanyo wa majukumu katika ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu.


Naye Mkurugenzi wa Shikuwata Magreth Mapunda, aliwataka washiriki hao kuwa watulivu na kufuatilia kwa makini mafunzo hayo, ambayo mwisho wa siku yatawasaidia kujua haki zao na kuwajengea uwezo wa kuweza kufuatilia masuala mbalimbali hususan serikalini na hata katika jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Diwani wa kata ya Namabengo Vitus Ngonyani, aliwataka wananchi kuwaona watu wenye ulemavu kama sehemu ya jamii ya Watanzania na wana haki sawa na watu wengine.

Ngonyani aliongeza kwa kuitaka jamii kuacha tabia ya kuwabagua na kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu, badala yake amewahimiza kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanapopambana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwasaidia fedha kwa ajili ya matibabu, usafiri, chakula na elimu.

Kwa upande wao walemavu hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa wanakabiliwa na matatizo hayo ikiwemo kutokuwepo kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali za taifa, ugumu wa kupata nafasi za ajira pindi zinapotokea, pamoja na kupata usumbufu mkubwa katika upande wa kupata matibabu pale wanapokwenda kutibiwa kwenye vituo vya afya au hospitali za serikali.

No comments: