Saturday, July 26, 2014

MKUU WA MKOA WA RUVUMA AMTAKA MKAGUZI WA NDANI HALMASHAURI YA MBINGA KUTIMIZA MAJUKUMU YAKE YA KAZI BILA KUINGILIWA

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu (watatu kutoka kushoto) nje ya ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amemuagiza Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kuhakikisha kwamba, anatoa taarifa sahihi na kwa wakati juu ya mwenendo wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi wilayani humo ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Sambamba na hilo aliwataka watendaji husika katika halmashauri hiyo kutoingilia utendaji kazi wa ofisi ya mkaguzi huyo, huku akisema kuwa ni ofisi ambayo ipo huru na inafanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yeyote.

"Sasa hivi ndugu zangu nahitaji mtambue kuwa ofisi ya mkaguzi wa ndani katika halmashauri ni idara kamilifu ambayo ipo huru, kwa hiyo ninachosema hapa mkaguzi fanya kazi zako bila kuingiliwa na mtu wewe una jukumu kubwa sana", alisema Mwambungu.

Mwambungu alitoa rai hiyo alipokuwa akihutubia leo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya Mbinga, lililofanyika kwenye ukumbi wa jumba la Maendeleo uliopo mjini hapa.

Aidha Mwambungu aliwataka Madiwani wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi, kwa kuhakikisha kuwa miradi ya wananchi inajengwa kwa viwango vinavyokubalika. (Value for money)

Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa mtendaji yeyote ndani ya halmashauri hiyo atakayeonekana anakikuka taratibu za utumishi wa umma kwa lengo la kujinufaisha yeye binafsi, atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

"Lazima muwe makini sana katika kazi zenu, muitendee haki nafasi mliyonayo, Madiwani simamieni majukumu yenu ya kazi ipasavyo katika kata zenu", alisisitiza.

Hata hivyo aliongeza kuwa ni muhimu kwa fedha zinazokusanywa kupitia ushuru wa aina mbalimbali, zirudi vijijini kwa wananchi katika kutekeleza miradi husika na sio kuishia mifukoni kwa wajanja wachache wenye nia mbaya ya kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

No comments: