Saturday, July 19, 2014

MAMA SALMA KIKWETE AWAPA SOMO AKINA MAMA MBINGA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

VIFO vinayotokana na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua hapa nchini, vimepungua kutoka akina mama 578 miaka ya nyuma na kufikia 454 mwaka huu kati ya vizazi hai 100,000 ambao walikuwa wakijifungulia nyumbani na kusababisha mtoto au mama kufariki dunia.

Upungufu huo umetokana na jitihada ya serikali kufanya kazi ya ujenzi wa zahanati vijijini na vituo vya afya kwa kila kata, ambapo akina mama wengi wajawazito huenda huko kwa ajili ya kupata huduma husika tofauti na kujifungulia majumbani.

Hayo yalisemwa leo na mke wa Rais hapa nchini, Mama Salma Kikwete alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Mama Salma alisema ujenzi wa vituo hivyo vya kutolea huduma za afya vijijini ulilenga kupunguza tatizo hilo, na kwamba ni ahadi iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi na ambayo ipo katika ilani yake.


“Ndugu zangu wanambinga ilani ya CCM imetekeleza ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, wakati huu sasa sio wakati tena wa mama mjamzito au motto kupoteza maisha ni wakati wa kwenda kujifungulia huko ili tuepukane na matizo yanayoweza kutokea baadaye”, alisema Mama Kikwete.

Aidha aliwataka akina mama hao kabla ya kujifungua wa wahi kliniki mapema kupima afya zao, kwa lengo la kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya Ukimwi au la ili waweze kufungua mtoto aliyesalama ambaye hana maambukizi ya ugonjwa huo.

“Kujua afya ndio kujua usalama wako, nendeni kliniki mkapime afya zenu ili kujua kama mna maambukizi lengo ni kumpata mtoto aliyekuwa salama”, alisisitiza. 

Pamoja na mambo mengine alisema baadhi ya akina mama wanapojifungua hupatwa na tatizo la ugonjwa wa fistula ambapo hutokwa na mkojo mfululizo, hivyo aliwataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma endapo kama kuna mama wa aina hiyo haraka apelekwe hospitali ili aweze kupatiwa matibabu kabla tatizo kuwa kubwa.

Mama Salma alifafanua kuwa baadhi ya kaya zikiona mama ana tatizo kama hilo hufikiri tofauti na kujiingiza katika mila potofu eti amerogwa, ambapo amekemea hali hiyo na kuagiza jamii iachane na mambo hayo.

No comments: