Saturday, July 19, 2014

BALOZI WA CHINA AMPONGEZA RAIS KIKWETE


Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

BALOZI wa China nchini Lu Youqing amempongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Kikwete kutokana na kazi yake kubwa, anayoifanya ya kusimamia shughuli za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami jambo ambalo litasaidia kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.

Pongezi hizo alizitoa wakati alipokuwa akiongea katika mkutano wa hadhara mjini hapa, mara baada ya Rais Kikwete kufungua rasmi barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Peramiho yenye urefu wa kilometa 78 ambayo imejengwa na kampuni ya SINOHYDRO ya nchini China.

Lu Youqing alisema kuwa watanzania wanapaswa kuendelea kuunga jitihada zinazofanywa na serikali yao, ili waweze kuondokana na umasikini wa kipato na kwamba serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.


Alisema kama nchi nataka kupata uchumi mzuri ni lazima kujenga barabara kwa kiwango kinachoridhisha kazi ambayo Tanzania imekuwa ikilitekeleza kwa manufaa ya wananchi wake, na kwamba ushahidi upo wazi kutokana na kila kona kuwepo kwa wakandarasi wanaoshughulikia ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Balozi huyo alisema  kwa kutumia barabara hizo wananchi wataweza kuuza mazao yao sokoni kiurahisi na hivyo kujikwamua kiuchumi na kwamba aliwaasa wananchi, kuepuka vitendo vya wizi katika barabara hiyo kwani kwa kufanya hivyo barabara itaharibika mapema.

Naye Waziri wa ujenzi John Magufuli alisema Rais Kikwete ataendelea kukumbukwa kutokana na juhudi zake za kutekeleza kwa vitendo ahadi zake alizozitoa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ambapo moja ya ahadi ambayo aliitoa ni ya ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Peramiho kwa kiwango cha lami ahadi ambayo imekamilika.

Magufuli alisema Wizara yake imekuwa ikitekeleza kwa vitendo yale yote ambayo yanaelekezwa na serikal, hivyo wananchi kwa upande wao nao hawana budi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo za kuwaletea maendeleo ili hatimaye lengo la kuondokana na umasikini liweze kupata mafanikio yaliyokusudiwa.
        



No comments: